1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi wachache kunufaika na nyongeza ya mshahara Kenya

12 Mei 2022

Muungano wa wafanyakazi nchini Kenya COTU umefurahishwa na ongezeko la asilimia 12 la kima cha chini cha mshahara, alichotangaza rais Uhuru Kenyatta katika sherehe ya Siku ya Wafanyakazi duniani.

https://p.dw.com/p/4BBkg
Afrika Kenia Arbeiten niedriger Lohnsektor
Picha: epa Jon Hrusa/dpa/picture-alliance

Muungano wa wafanyakazi nchini Kenya COTU umefurahishwa na ongezeko la asilimia 12 la kima cha chini cha mshahara, alichotangaza Rais Uhuru Kenyatta, mnamo mei mosi katika sherehe ya Siku ya Wafanyakazi duniani. 

Ongezeko la asilimia 12 la kima cha chini cha mshahara nchini humo limekuja katika wakati ambapo nchi hiyo ya Afrika Mashariki inakabiliwa na mfumuko wa bei, japo wafanyakazi wachache tu ndio watakaofaidika na ongezeko hilo.

Soma pia: Tanzania: Wananchi walalamika kukosa bidhaa muhimu

"Ni furaha kwa wafanyakazi nchini Kenya hasa ​​katika wakati ambapo mishahara ya wafanyakazi haijapandishwa tangu uwepo wa janga la ugonjwa wa UVIKO-19." alisema Barasa Adams, mshauri wa kimataifa wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi.

Mara ya mwisho mishahara iliongezwa kwa asilimia 5 ilikuwa ni miaka mitatu iliyopita. "Tumefurahi sana kuwa rais ameongeza asilimia 12 kwa sababu hatukutarajia," Adams aliiambia DW.  

Chama cha waajiri Kenya (FKE) hakijafurahishwa na uamuzi wa kupandisha mishahara

Afrika Kenia Arbeiten niedriger Lohnsektor
Wafanyibiashara katika soko la maua mjini Naivasha.Picha: Zhang Yu/Xinhua News Agency/picture alliance

Chama cha waajiri Kenya (FKE), ambacho kinajumuisha waajiri wa sekta binafsi na umma, kilisema hali ya sasa ya uchumi nchini Kenya hairuhusu nyongeza ya mishahara.

"Hatujafurahishwa na ongezeko la mshahara kama waajiri na wafanyabiashara kwa sababu limekuja katika wakati mgumu kwa jumuiya ya wafanyabiashara na wafanyakazi," Mkurugenzi Mtendaji wa FKE Jacqueline Mugo ameiambia DW.

Kenya ndio nchi yenye mishahara ya juu zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki lakini takribani watu milioni 17 walioajiriwa nchini humo hawatanufaika moja kwa moja na nyongeza hiyo ya mishahara.

Hii ni kwa sababu sheria za kima cha chini cha mishahara hushughulikia tu wafanyikazi katika sekta rasmi, ambapo ni asilimia 17 tu ya wafanyikazi.

"Zaidi ya asilimia 80 ya watu hufanya kazi katika sekta isiyo rasmi, hivyo nyongeza ya mishahara haitawanufaisha kwa sababu sekta isiyo rasmi ni kubwa na sio lazima kufuata miongozo hii," alisema Ken Gichinga, mchumi mkuu wa shirika la ushauri la Mentoria Economics lilipo mjini Nairobi.

Soma pia: Mfumuko wa bei waongezeka zaidi nchini Sudan

Zaidi ya vibarua wawili kati ya watano walilipwa kima cha chini cha mishahara yao kulingana na Wakala wa Maendeleo wa Baraza la Vyama vya Wafanyakazi wa Denmark.

Hali ni mbaya zaidi kwa wafanyakazi ambao ni makundi maalumu, kama vile wanawake. Zaidi ya wafanyakazi wanne kati ya watano wa nyumbani walilipwa chini ya kima cha chini cha mshahara, kulingana na utafiti wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi COTU mwaka 2017.

Gharama ya maisha imepanda kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine

Warten auf Hilfsflotte in Gaza
Bei ya vyakula na mafuta imepanda maradufuPicha: AP

Gharama ya mahitaji muhimu kama vile mafuta, mahindi, mkate na maziwa, na usafiri imepanda sana katika miaka michache iliyopita nchini Kenya, kutokana na  janga la UVIKO-19 na hivi karibuni uvamizi wa Urusi nchini Ukraine pia umepelekea ugumu wa maisha kwa raia wengi nchini Kenya.

Lakini mchumi Ken Gichinga anasema kupanda kwa mishahara kunaweza kukosa tija kwa sababu biashara ambazo zinaporomoka kwa sababu ya majanga na gharama kubwa za uzalishaji, zinaweza kuajiri watu wachache.

Soma pia: China imeleta bidhaa, barabara, sasa Afrika yataka ajira

"Ikiwa unamiliki mgahawa na uliajiri wahudumu watano, unaweza kusema, nahitaji wahudumu watatu tu kwa kuwa kima cha chini cha mshahara kimepanda. Kupanda kwa mishahara kunaweza kuchangia zaidi ukosefu wa ajira kwa namna hiyo," alisema.

Hili linaungwa mkono na utafiti wa Washirika wa Sera ya Kiuchumi ya 2017 kuhusu kima cha chini cha mishahara nchini Kenya, ambapo uligundua kuwa wafanyakazi wa mashambani ni miongoni mwa watu maskini zaidi nchini Kenya kutokana na nyongeza ya kima cha chini cha mishahara iliyopelekea kuajiri wafanyakazi wachache.