1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyabiashara wa Haiti walilia kuchelewa polisi wa Kenya

18 Aprili 2024

Wafanyabiashara wa Haiti wameelezea hofu kubwa waliyonayo kuhusu kuchelewa kuwasili kwa ujumbe wa kulinda amani unaoongozwa na Kenya nchini humo ili kupambana na magenge ya uhalifu.

https://p.dw.com/p/4euy8
Rais William Ruto wa Kenya
Rais William Ruto wa Kenya, ambaye nchi yake hadi sasa haijapeleka kikosi cha kimataifa cha polisi kulinda amani nchini Haiti.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Katika barua iliyotumwa kwa Rais William Ruto wa Kenya, viongozi wa mabaraza manane ya juu ya biashara wamesema wana wasiwasi kwamba kikosi cha polisi cha kimataifa kinachoongozwa na Kenya bado hakijapelekwa zaidi ya miezi sita baada kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa, huku muda ulioafikiwa ukikaribia kuisha.

Soma zaidi: Haiti hatimaye yaunda rasmi Baraza tawala la mpito

Kenya, ndiyo nchi pekee iliyojitolea kuongoza ujumbe huo, lakini kufikia mwezi Machi ilikuwa bado haijawasilisha barua kwa Umoja wa Mataifa kuelezea rasmi mchango wake.

Haya yanajiri huku magenge yenye silaha yakizidisha mashambulizi yao katika sehemu za mji mkuu, Port-au-Prince.

Bandari imefungwa kwa zaidi ya mwezi mmoja, hali inayozuia usambazaji wa chakula na bidhaa muhimu huku mamilioni wakikabiliwa na njaa.