1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili waahidi dola bilioni 1.2 kwa Afghanistan

14 Septemba 2021

Mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa anasema ahadi za dola bilioni 1.2 zimetolewa kwa ajili ya kuwasaidia Waafghani wanaokabiliwa na mzozo wa kiutu unaozidi nchini humo na katika ukanda huo mzima.

https://p.dw.com/p/40HGC
Grenze Afghanistan - Pakistan | Flüchtlinge aus Afghanistan
Picha: Saeed Ali Achakzai/REUTERS

Mkuu huyo Martin Griffiths amesema ahadi hizo ni hatua muhimu ya kuwasaidia wanaohitaji misaada.

Griffiths ameyasema haya mwishoni mwa mkutano wa ngazi ya juu mjini Geneva, uliokuwa unatafuta pia dola milioni 606 hadi mwishoni mwa mwaka kwa ajili ya kuwasaidia watu milioni 11. Mkuu huyo amesema fedha hizo za ziada zimo katika hiyo ahadi ya dola bilioni 1.2.

Griffiths sasa ametoa wito kwa wafadhili kufanya ahadi zao kuwa kweli haraka iwezekanavyo kwa kutoa fedha walizoahidi. Anasema zitawasaidia pakubwa Waafghani hasa wanawake.

"Jukumu la wanawake na wasichana ni muhimu mno kama sehemu yoyote ile. Wanastahili kupata elimu, wanastahili kupata haki zao na huduma zengine muhimu kama ilivyo kwengineko duniani," alisema Griffiths.

Misaada ya kiutu si suluhisho la matatizo ya Afghanistan

Wito wa kuchangishwa fedha kwa ajili ya Afghanistan ulitolewa kutokana na hofu kwamba raia wengi wanakabiliwa na utapia mlo na ukosefu wa chakula nchini humo, huku wengi wengine wakiwa wameyakimbia makaazi yao na kipindi cha majira ya baridi kikiwa kinakaribia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kutia fedha katika uchumi wa Afghanistan ili kuzuia kuanguka kwa uchumi huo, jambo litakalokuwa na athari kwa raia. Kulingana na Guterres misaada ya kiutu haitotatua matatizo, iwapo uchumi utaanguka ingawa inaweza kutumika kusukuma ajenda ya haki za binadamu nchini humo.

"Iwapo tunataka kulinda haki za binadamu za Waafghani, njia bora ni kuendelea kutoa misaada ya kiutu na kutumia misaada hiyo kuzungumza na Taliban na kusukuma suala la kutekelezwa kwa haki," alisema Guterres.

Taliban wanafanya mauaji ya kulipiza kisasi kwa waliokuwa maafisa wa usalama

Naye mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na Haki za Binadamu Michelle Bachelet amesema afisi yake imepokea madai ya kuaminika ya mauaji ya kulipiza kisasi ya maafisa wa zamani wa usalama nchini Afghanistan yanayofanywa na Taliban.

Schweiz | UN Menschenrechtsrat | Michelle Bachelet
Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle BacheletPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Akizungumza katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa,Bachelet amesema pia maafisa katika serikali iliyopita ya Afghanistan pamoja na familia zao wanakamatwa na kuzuiliwa na baadae wanapatikana wakiwa wamefariki.

Mkuu huyo ametahadharisha kwamba kutakuwa na ukurasa mpya na mbaya kwa Afghanistan kutokana na kukosekana uwiano kati ya maneno ya Taliban na vitendo vyao.

Vyanzo: AFPE/APE