Marekani yahofia Al-Qaeda kuibuka tena nchini Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yahofia Al-Qaeda kuibuka tena nchini Afghanistan

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amesema kundi lenye itikadi kali la Al-Qaeda ambalo liliitumia Afghanistan kama kituo cha kuishambulia Marekani miaka 20 iliyopita, linaweza kujaribu kuibuka tena nchini humo.

Austin ameyasema hayo katika mji wa Kuwait alipokuwa akikamilisha ziara yake ya siku nne katika mataifa ya Ghuba ya Uajemi. Ameongeza kuwa Marekani imejipanga kuzuia kurejea kwa Al-Qaeda nchini Afghanistan hali itakayoleta kitisho kwa Washington.

"Ninafikiri! unajua kulingana na asili ya Al-Qaeda na ISIS-K ni kwamba, watajaribu kila wakati kutafuta sehemu ya kukua na kuibuka tena, iwe huko, iwe Somalia, ama katika sehemu yoyote isiyoongozwa. Ninafikiri hiyo ndio asili ya kundi hilo".

Kundi la Taliban liliwahi kulihifadhi kundi la Al-Qaeda wakati wa utawala wake wa Afghanistan wa mwaka 1996 hadi 2001. Uvamizi wa Marekani uliliondoa kundi la Taliban madarakani baada ya kukataa kuwakabidhi viongozi wa Al-Qaeda kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 huko Marekani.

Katika kipindi cha miaka 20 ya vita ya Marekani, kundi la Al-Qaeda lilitoweka, lakini sasa kumeibuka maswali juu ya mustakabali wake wakati ambao Taliban wamerejea mamlakani mjini Kabul. Austin amesisitiza kwamba jeshi la Marekani lina uwezo wa kulizuia kundi la Al-Qaeda au kundi jingine lenye itikadi kali ambalo ni kitisho kwa Washington kwa kutumia mashambulizi ya angani kutokea eneo lolote ikiwemo Ghuba ya Uajemi. Lakini amekiri kwamba inaweza kuwa vigumu zaidi bila ya kuwepo na majeshi yake na timu ya Intelijensia huko Afghanistani.

Kuwait | Lloyd Austin trifft Scheich Nawaf al-Ahmad al-Dschabir as-Sabah

Waziri Lloyd Austin akiwa na Emir wa Kuwait Nawaf Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah

Austin na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antonyl Blinken walionekana kwa pamoja siku ya Jumanne nchini Qatar katika ishara ya kuonyesha shukrani kwa mataifa yote ya Ghuba jinsi yalivyosaidia kusafirisha maelfu ya Waafghani na watu wengine waliohamishwa kutoka Kabul. Blinken pia alitembelea kituo cha kuwahamisha watu hapa Ujerumani na Austin pia alizuru huko Bahrain na Kuwait.

Hayo yakijiri serikali mpya ya Taliban imekubali kuruhusu zoezi la kuwahamisha Wamarekani 200 na raia wengine wa kigeni ambao bado wamesalia Afghanistan. Kuondolewa huko kutakuwa miongoni mwa safari za kwanza za ndege za kimataifa kutoka uwanja wa ndege wa Kabul tangu kundi hilo lilipochukua madaraka katikati ya mwezi Agosti.

Hatua hiyo inakuja siku mbili baada ya Taliban kutangaza serikali ya mpito ambayo imeundwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa kabila la Pashtuni wakiwemo washukiwa wa ugaidi na Waislamu walio na misimamo mikali na kuondoa matumaini ya jamii ya kimataifa ya utawala ulio na misimamo ya wastani.