Umoja wa Mataifa waitisha mkutano kuisadia Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Mataifa waitisha mkutano kuisadia Afghanistan

Umoja wa Mataifa umeitisha mkutano wa wafadhili utakaofanyika Jumatatu kuchangisha fedha za kuisadiia Afghanistan, kiasi wiki tatu tangu kundi la wapiganaji wa Taliban lilipochukua udhibiti wa taifa hilo.

Umoja wa Mataifa unalenga kutumia mkutano huo wa Jumatatu kupigia debe uchangishaji wa dola milioni 606 zinazohitajika kabla ya mwezi Disemba kuwasaidia Waafghani wanaokabiliwa na hali mbaya ya mzozo wa kibinadamu.

Zaidi ya mawaziri 40 kutoka mataifa mbalimbali duniani wamethibitisha kushiriki mkutano huo wa mjini Geneva utakaohudhuriwa pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Mashirika ya umoja wa mataifa tayari yametahadhrisha kuwa hali ya upatikanaji  huduma muhimu nchini Afghanistan imefikia kiwango cha chini na msaada unahitajika haraka kunusuru Maisha ya watu wanaokabiliwa na madhila.

Kwa sehemu kubwa msaada huo wa kifedha utatumika kutoa huduma za afya, chakula, usambazaji wa maji ya kunywa na miradi ya usafi wa mazingira.

Umoja wa Mataifa umesema fedha zinahitajika haraka hususan zitakazotumika kugawa chakula, ukitahahdrisha kwamba zaidi ya asilimia 93 ya wakaazi wa nchi hiyo hawana chakula cha kutosha.

Umoja wa Mataifa unalenga kutumia mkutano huo wa leo kupigia debe uchangishaji wa dola milioni 606 kuwasaidia Waafghani.

Umoja wa Mataifa unalenga kutumia mkutano huo wa leo kupigia debe uchangishaji wa dola milioni 606 kuwasaidia Waafghani.

Mbali ya huduma muhimu za jamii fedha hizo zitaelezekwa pia katika ujenzi wa makaazi ya muda kwa watu milioni 3.5 waliopoteza maskani zao kutokana na machafuko ya miaka mingi nchini Afghanistan.

Kadhalika Umoja wa Mataifa unanuwia kutumia michango itakayopatikana kuongeza msaada kwa mashirika ya kiraia yanayounga mkono ustawi wa wanawake, watoto na sekta ya elimu nchini Afghanistan

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR

Filippo Grandi alionya jana Jumapili kwamba iwapo kutatokea mapigano mapya, ukiukaji wa haki za binadamu au kuanguka kwa hali ya uchumi na huduma za jamii, waafghani wengi huenda watajaribu kuikimbia nchi hiyo na kuzusha mzozo mkubwa wa uhamiaji.

Kuelekea mkutano wa leo, mataifa mengi yameonesha nia ya kutoa mchango lakini yana wasiwasi na jinsi msaada huo utakavyotumika ikitiliwa maanani kwamba Taliban ndiyo wanaongoza serikali. Wengi ya wawakilishi wa mataifa ya magharibi wametaka kuwe na mashrti makali juu ya matumizi ya msaada utakaopatikana.

Nchini Afghanistan kwenywee inaarifiwa kuwa hali ya usalama bado ni shwari lakini raia wengi wanalalamika kuhusu kupanda kwa bei za vyakula, kudorora kwa shughuli za uchumi na ukosefu wa nafasi za kazi.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi

Katika kile kinachoashiria kuwa maisha yanarejea taratibu kwenye hali ya kawaida, ndege ya abiria ya safari ya kimataifa iliyowasili kutoka Pakistan iliruka leo asubuhi mjini Kabul kurejea Islamabad, ikiwa ni ya kwanza tangu Taliban ilipochukua udhibiti.

Kurejea kwa ndege za abiria itakuwa kipimo muhimu kwa kundi hilo linaloegemea siasa ya kiislamu ambalo liliahidi kuwaruhusu Waafghani wenye nyaraka halali kuondoka kwa uhuru nchini humo.

Katika hatua nyingine Urusi imetangaza leo kuwa inapeleka msaada wa chakula na dawa nchini kama sehemu ya mchango wake wa kiutu kwa taifa hilo.

Mataifa mengi ikiwemo Urusi yalipokea kwa tahadhari ushindi wa Taliban na serikali mpya iliyoundwa na kundi hilo inayojumuisha viongozi wengi wahafidhina.

Mwandishi: Rashid Chilumba/dpa/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga