1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wachezaji 10 wa kufuatilia Kombe la Dunia 2026

29 Mei 2026

Kutoka Messi na Ronaldo hadi Yamal na Mbappé, Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kushuhudia mchanganyiko wa mastaa wakongwe na kizazi kipya cha nyota wa soka, huku Messi na Ronaldo wakitarajiwa kun'gara zaidi.

https://p.dw.com/p/5EVFW
Soka | Maadhimisho ya miaka 40 ya kuzaliwa kwa Cristiano Ronaldo
Lionel Messi wa Argentina, kushoto, akiwa karibu na Cristiano Ronaldo wa Ureno kabla ya mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa katika Uwanja wa Old Trafford, Manchester, Uingereza, Novemba 18, 2014Picha: Jon Super/AP Photo/picture alliance

Kombe la Dunia 2026 linaweza kuwa jukwaa la mwisho kwa baadhi ya magwiji wakubwa wa soka duniani huku kizazi kipya kikijiandaa kuchukua nafasi yao.

Miongoni mwa wachezaji watakaovuta macho ya mashabiki ni Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, ambao huenda wakacheza Kombe lao la Dunia la mwisho.

Wakati huo huo, nyota chipukizi kama Lamine Yamal wanaonekana kuwa tayari kurithi enzi mpya ya soka la dunia.

Hawa hapa wachezaji 10 wanaotarajiwa kuwa gumzo katika mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Messi na Ronaldo bado hawajamaliza safari

Messi aliandika historia mwaka 2022 alipoiwezesha Argentina kutwaa Kombe la Dunia na kutimiza ndoto kubwa zaidi ya maisha yake ya soka.

Sasa akiwa na miaka 38, bado ana nafasi ya kuongeza urithi wake ikiwa ataiongoza Argentina kutetea taji hilo.

Kwa upande wake, Ronaldo mwenye miaka 41 bado anasaka taji pekee ambalo halijawahi kuingia katika kabati lake la mafanikio — Kombe la Dunia.

Mechi ya Kirafiki ya Soka 2026 | Hispania dhidi ya Misri | Lamine Yamal akiwa uwanjani
Nyota chipukizi kama Lamine Yamal wanaonekana kuwa tayari kurithi enzi mpya ya soka la dunia.Picha: Felipe Mondino/ZUMA/IMAGO

Nahodha huyo wa Ureno tayari ameshinda karibu kila taji kubwa katika ngazi ya klabu na timu ya taifa, lakini bado ana hamu ya kuandika historia nyingine.

Mbappé, Yamal na Haaland waongoza kizazi kipya

Kylian Mbappe bado anatajwa kuwa mrithi mkuu wa Messi na Ronaldo.

Mshambuliaji huyo wa Real Madrid tayari ameshinda Kombe la Dunia akiwa na Ufaransa mwaka 2018, lakini bado anatafuta Ballon d'Or na taji la Ligi ya Mabingwa ili kuimarisha hadhi yake.

Erling Haaland wa Norway naye anajiandaa kwa mashindano yake makubwa ya kwanza katika ngazi ya timu ya taifa baada ya kuvunja rekodi nyingi akiwa na Manchester City.

Kwa upande wa Yamal, nyota huyo wa Hispania tayari ameonyesha uwezo wake baada ya kung'ara katika Euro 2024 akiwa bado kijana mdogo sana.

Wengi wanaamini ndiye mwenye nafasi kubwa zaidi ya kuwa sura mpya ya soka la dunia katika miaka ijayo.

Kombe la Dunia 2022 | Fainali | Argentina dhidi ya Ufaransa | Kylian Mbappé akipokea Kiatu cha Dhahabu
Kylian Mbappe bado anatajwa kuwa mrithi mkuu wa Messi na RonaldoPicha: Marcio Machado/MIS International/IMAGO

Wachezaji wengine wa kuangaliwa kwa karibu

Ousmane Dembele anaingia kwenye mashindano hayo akiwa mmoja wa wachezaji bora duniani baada ya kufufua kiwango chake akiwa PSG.

Jude Bellingham wa England ataongoza matumaini ya Waingereza ya kutwaa taji lao la kwanza kubwa tangu mwaka 1966.

Neymar atakuwa akisaka ndoto yake ya kuiongoza Brazil kutwaa Kombe la Dunia la sita katika historia yake.

Kwa upande wa Afrika, macho mengi yatakuwa kwa Mohamed Salah, ambaye ataongoza matumaini ya Misri katika mashindano hayo.

Nchini Marekani, mwenyeji wa mashindano, Christian Pulisic anatarajiwa kuwa nyota mkubwa wa timu ya taifa ya Marekani chini ya kocha Mauricio Pochettino.

Ligi ya Mabingwa Ulaya 2025/26 | Nusu Fainali | Bayern Munich dhidi ya PSG | Ousmane Dembélé akishangilia bao lake
Ousmane Dembele anaingia kwenye mashindano hayo akiwa mmoja wa wachezaji bora duniani baada ya kufufua kiwango chake akiwa PSGPicha: Jean Catuffe/DPPI media/picture alliance

Kwa mchanganyiko wa magwiji wanaokaribia mwisho wa safari zao na vipaji vipya vinavyochipukia, Kombe la Dunia 2026 linaonekana kuwa moja ya mashindano yatakayobeba hadithi nyingi zaidi katika historia ya soka.