1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge nchini Uingereza wamuangusha tena Boris Johnson

Saumu Mwasimba
5 Septemba 2019

Wabunge waunga mkono muswaada unaoizuia Uingereza kujitowa katika Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano mwishoni mwa mwezi Oktoba,hatua inayomfanya boris Johnson sasa kutaka kuungwa mkono na umma kuitisha uchaguzi mkuu

https://p.dw.com/p/3P3EF
Brexit Debatte im britischen Unterhaus
Picha: picture alliance/dpa/AP/House Of Commons/J. Taylor

Wabunge wa Uingereza jana walipiga kura kuunga mkono muswaada wa sheria ya kuizuia Uingereza kujiondowa Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano mwishoni mwa mwezi Oktoba.Hatua ya wabunge imedhihirisha  kwamba mkakati wa waziri mkuu Boris Johnson wa kutaka uchaguzi mkuu wa kabla ya wakati umegonga mwamba.

Wabunge kwa mara nyingine wamempa pigo kubwa waziri mkuu Boris Johnson baada ya kuamua kuunga mkono muswada unaoilazimisha Uingereza kutojitowa katika Umoja wa Ulaya bila ya makubaliano Oktoba 31 na badala yake sasa nchi hiyo inaamanisha itabidi irefushe mchakato wa Brexit hadi Januari 31 mwaka 2020 ikiwa hakuna makubaliano mapya yatakayoidhinishwa na bunge pamoja na Umoja wa Ulaya kufikia Oktoba 19.

London: Brexit
Picha: picture-alliance/AP/J. Taylor

Wabunge 327 waliuunga mkono muswaada unaokwenda kinyume na matakwa ya Boris Johnson na 299 walisimama kuupinga. Kwa maneno mengine Boris Johnson ameshindwa kupata wingi wa thuluthi mbili za kumuwezesha kuitisha uchaguzi wa mapema na  sasa Muswaada huo utapelekwa mbele ya baraza kuu la wajumbe kabla ya kuwa sheria na kuidhinishwa na Malkia.

Ni mara ya tatu kushindwa bungeni waziri mkuu huyo ndani ya siku mbili lakini anasema wabunge wamefanya kosa kubwa.

''Ni muswaada ambao bila shaka umeshayafikisha mwisho majadiliano,muswaada ambao ni wazi unarefusha muda wa kujitowa umoja wa Ulaya mpaka mwakani au pengine baada ya miaka mingi ijayo,na pia ni muswaada unaoifanya Uingereza kuwajibika kufuata kinachoamrishwa  na Brussels,na kuwapa washirika wetu udhibiti.Lakini pia ni muswaada ulioundwa kuyapindua maamuzi ya kidemokrasia ya  wananchi katika kura ya maoni iliyopigwa 2016.''

Politics and Westminster
Picha: picture-alliance/Zumapress/D. Haria

Nje ya bunge la Uingereza wananchi wanaounga mkono nchi yao ibakie kwenye Umoja wa Ulaya walipiga kambi na punde baada ya matokeo ya kura kutangazwa kila mmoja alikuwa na lake la kusema Cliff Dartnaw yeye alisema hivi

''Nataraji Boris Johnson amejionesha jinsi alivyokuwa ni mwanasiasa asiyekuwa na lake jambo anajaribu kuipeleka nchi hii katika mkondo mbaya kabisa.''

Sasa waziri mkuu Johnson anatafuta njia nyingine mpya za kufanikisha uchaguzi wa mapema ufanyike  na ofisi yake imeshasema kwamba kiongozi huyo atawageuka wananchi kutafuta uungwaji mkono wa mkakati wake huo wa kutaka uchaguzi ufanyike wiki kadhaa zijazo.

Imesikika kutoka Downing Street kwamba Johnson anataka leo leo kuzungumza moja kwa moja na umma wa Uingereza ingawa maelezo ya kina juu ya hotuba au mkutano anaopanga kuufanya hayajatolewa.Umoja wa Ulaya unawasiwasi na msimamo wa Boris Johnson.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Daniel Gakuba