Waasi wachukuwa kambi ya kijeshi Myanmar | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

MYANMAR

Waasi wachukuwa kambi ya kijeshi Myanmar

Wakati maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi yakiendelea nchini Myanmar, kundi la waasi limekiteka kituo cha kijeshi mashariki mwa nchi hiyo katika wakati mataifa ya kusini mwa Asia yakisaka suluhisho la kisiasa.

Mapigano yalizuka kwenye eneo la mashariki linalopakana na Thailand, ambako kundi la waasi wa jamii ya wachache ya Karen lilikivamia kituo kimoja cha kijeshi, yakiwa mapambano makali kabisa tangu jeshi kunyakuwa madaraka tarehe 1 Februari na kuiingiza Myanmar kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa na kiusalama.

Karen National Union (KNU), moja ya makundi makongwe kabisa ya waasi nchini humo, lilisema lilikuwa limeichukuwa kambi hiyo ya kijeshi kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Salween, ambao unazitenganisha Myamnar na Thailand.

Wanavijiji walio upande wa Thailand waliripoti kusikia milio ya bunduki kabla ya jua kuchomoza hivi siku ya Jumanne (27 Aprili). Picha za vidio zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha moto na moshi kutokea kwenye eneo hilo lenye vilima na misitu.

Myanmar | Militärtraining bei der Karen National Union (KNU)

Wapiganaji wa kundi la Karen National Union

Msemaji wa masuala ya nje ya kundi hilo, Saw Taw Nee, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba vikosi vyao vilichukuwa udhibiti wa kambi hiyo majira ya saa kumi na moja alfajiri.

"Kambi nzima imechukuliwa na kuchomwa moto na sasa wapiganaji wetu wanatafuta maiti na majeruhi", alisema Saw akiongeza kwamba kulikuwa na mapigano kwenye maeneo mengine, ingawa hakueleza kwa undani zaidi.

Muafaka dhaifu wa ASEAN na watawala wa kijeshi

Mapigano hayo yanatokezea wakati utawala wa kijeshi ukisema uko tayari kufikiria mapendekezo yaliyotolewa na Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) baada ya mkutano wa mwishoni mwa wiki nchini Indonesia.

Indonesien Präsident Joko Widodo

Rais Joko Widodo wa Indonesia (wa pili kushoto) akitowa tamko la Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) juu ya mzozo wa Mnyamar tarehe 24 Aprili 2021.

Kwa mujibu wa viongozi wa jumuiya hiyo, walikuwa wameafikiana na utawala wa kijeshi kukomesha mashambulizi dhidi ya waandamanaji na kuitisha mazungumzo kati yake na upinzani.

Hata hivyo, utawala huo wa kijeshi ulisema ungelichukuwa hatua hizo baada ya kwanza "hali kurejea kuwa ya kawaida na kwa maslahi ya watu wa Myanmar."

Lakini viongozi wa ASEAN walikosolewa vikali na wapinzani kwa kuualika utawala huo wa kijeshi, wakisema kwamba mualiko wao uliashiria kuitambua serikali iliyo haramu na kwa kushindwa kutowa wito wa kuachiliwa kwa kiongozi mkuu wa upinzani, Aung San Suu Kyi, na wenzake zaidi ya 3,400 wanaoshikiliwa na jeshi tangu Februari Mosi. 

Maelfu ya watu wamejitokeza leo mitaani katika maeneo mbalimbali ya nchi kwenye maandamano ya kuupinga utawala huo na kuonesha mshikamano wao na serikali kivuli inayoundwa na chama cha NLD kilichoondoshwa madarakani na kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi.