1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wapokea tuzo kwa ushujaa wao

Josephat Charo22 Novemba 2007

Takriban waandishi 500 wa habari wameuwawa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Hayo ni kwa mujibu wa shirika linalowalinda waandishi wa habari la CPJ, lililo na makao yake makuu mjini New York nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/CRXy
Wanachama wa shirika la waandishi wa habari wasio mipaka wakiandamana mjini Beijing ChinaPicha: AP

Shirika la kuwalinda waandishi wa habari la kimarekani, CPJ, Jumanne iliyopita liliwaenzi waandishi watano wa habari walioonyesha ushujaa dhidi ya kubanwa uhuru wa kutangaza habari, kwa kuwapa tuzo ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari ya mwaka huu wa 2007.

Katika nchi ambazo nne kati ya tano wanakotokea washindi wa tuzo hiyo, zikiwemo Russia, China, Pakistan na Mexico, kumekuwepo mauaji ya waandishi wa habari. Waandishi wameuwawa na wengine kupotea katika nchi zote nne na washindi wote wa tuzo ya mwaka huu wamekuwa wahanga wa mateso na ukandamizaji.

Mmoja wa washindi, Adela Navarro Bello, mwanamke mwenye umri wa miaka 39,ameliambia shirika la habari la IPS kwamba tatizo kubwa nchini Mexico ni wauaji kutochukuliwa hatua yoyote kisheria. Hali hiyo inawaweka katika hatari ya kushambuliwa.

´Mtu anapomshambulia mwandishi wa habari nchini Mexico, basi unajua hataadhibiwa,´ ameongeza kusema Navarro Bello.

Bello ni mkurugenzi mtendaji wa jarida la Zeta linalochapishwa kila wiki katika mji wa mpakani wa Tijuana nchini Mexico.

Jarida hilo lilianzishwa mnamo mwaka 1980, na ni gazeti pekee linalochapisha makala kuhusu uchaguzi wa visa vya uhalifu unaopangwa, uuzaji wa dawa za kulevya na kesi za ufisadi katika majimbo ya kaskazini mwa Mexico, uhuru wa kuripoti habari hubanwa mara kwa mara.

Jarida la Zeta ambalo lina historia ya kuchapisha habari kuhusu uhalifu katika mpaka wa Marekani na Mexico, ni la kusisimua lakini wakati huo huo linahuzunisha.

Aliyesaidia kuliasisi jarida hilo, Hector Felix Miranda, aliuwawa mnamo mwaka wa 1988 na mhariri mwandamizi Francisco Ortiz Franco akauwawa mwaka wa 2004.

Mnamo mwaka wa 1997, baada ya jaribio la kumuua J Jesus Blancornelas, muasisi na mkurugenzi wa jarida la Zeta, ambapo mmoja wa walinzi wake aliuwawa, viongozi wa Mexico walimpa mwandishi wa habari, Navarro Bello, kizibao kisichoweza kutobolewa kwa risasi pamoja na walinzi wawili. Hata hivyo hayo yote yakamsumbua mwandishi huyo wa habari.

Nchini Pakistan aina nyingine ya hatari imeanza kujitokeza. Rais Pervez Musharraf amekuwa akiwakandamiza waandishi wa habari wanaoukosoa utawala wake tangu alipotangaza utawala wa hali ya hatari nchini humo mwanzoni mwa mwezi huu. Lakini waandishi wa habari kama vile Mazhar Abbas wamekuwa wakiilinda haki ya Wapakistan kupata habari.

Mazhar Abbas ni naibu mkurugenzi wa televisheni ya ARY World, inayotangaza kwa saa 24 katika lugha ya kiurdu na kihindi nchini Pakistan. Abbas pia ni katibu mkuu wa chama cha waandishi wa habari nchini humo. Alikataa kuwacha kazi yake hata licha ya vitisho vya mara kwa mara kwamba atauwawa pamoja na familia yake.

Mwezi Mei mwaka huu alikuwa mmoja wa waandishi wa habari waliopata risasi ndani ya bahasha nyeupe zilizotundikwa kwenye magari yao walipotoka kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Karachi uliomalizika usiku.

Alikuwa katika orodha ya watu wanaowindwa na baraza la Mohajir Rabita, kikundi cha kisiasa cha kikabilia katika mkoa wa kusini wa Pakistan, chenye mafungamano na rais Pervez Musharraf.

Kama ripota wa shirika la habari la AFP mjini Karachi, Mazhar Abbas aliripoti kutekwa nyara kwa mwandishi wa jarida la Wall Street, Daniel Pearl, mnamo mwaka wa 2002 na baadaye uchunguzi na kesi.

Dmirtry Muratov, aliyewapoteza maripota watatu wa gazeti lake la Novaya Gazeta linalochapishwa mjini Moscow nchini Urusi, amesema alifikiria kulifunga gazeti hilo, lakini akaendelea kuchapisha habari kwa sababu mamilioni ya wasomaji wa gazeti hilo wanaunga mkono maadili ya demokrasia ya kweli.

Gazeti la Novaya ni gazeti pekee lenye ushawishi wa kitaifa nchini Urusi kwa wakati huu. Muratov alilianzisha gazeti hilo mwaka wa 1993 na bado ni nguzo muhimu katika uchapishaji wa gazeti hilo. Kutoka kashfa kubwa za rushwa, matumizi mabaya ya mamlaka hadi ukiukaji wa haki za binadamu, gazeti hilo limeripoti kuhusu siri za serikali ya rais wa Urusi, Vladamir Putin.

Lakini gazeti hilo limelipa gharama kubwa kwa kifo cha mwandishi wa habari aliyejihusisha na maswala ya uchunguzi, Anna Politkovskaya.

Mshindi wa mwisho wa tuzo ya shirika la CPJ ni Gao Qinrong, aliyemaliza kifungo cha miaka minane gerezeni nchini China. Mwandishi huyo hakuweza kuhudhuria sherehe za kutolewa kwa zawadi hizo kwa sababu serikali ya China ilimkataza pasi ya kusafiria.

Gao aliripoti kuhusu rushwa katika mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika mkoa wa Shanxi nchini China.

Tom Brokaw, mtangazaji wa habari wa televisheni ya NBC, ripota na mwandishi wa vitabu, alipokea tuzo ya kumbukumbu ya Burton Benjamin ya shirika la CPJ kwa ufansi alioupata katika maisha yake. Mwenyekiti wa shirika linalowalinda waandishi wa habari la CPJ alitangaza kuwa kitita cha dola milioni moja za kimarekani zinahitajika kuuimarisha mtandao wa shirika hilo duniani kote, unaojulikana kwa jina International Programme Network. Tayari karibu dola 750,000 zimetolewa kulifikia lengo hilo.

Zaidi wa watu 900 walihudhuria chakula cha jioni kilichoandaliwa kuchangisha fedha. Jumla ya dola milioni 1.4 zilitolewa hivyo kuweka rekodi mpya ikilinganishwa na mikutano mingine ya michango.

Brian Williams, mtangazaji, mkurugenzi wa televisheni ya NBC na mwanachama wa bodi ya shirika la CPJ, aliandaa chakula hicho cha jioni katika hoteli ya Waldorf Astoria mjini New York.