Waandamana kushinikiza hatua za kunusuru dunia. | Masuala ya Jamii | DW | 07.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Waandamana kushinikiza hatua za kunusuru dunia.

Wanaharakati wa vuguvugu la kupigania mazingira wameanza maandamano kwa kuzuia barabara kuu mjini Berlin na Amsterdam, katika kile wanachokiita mfululizo wa maandamano ya kushinikiza sera mpya kuhusiana na mazingira. 

Waandamanaji kama hao wameingia mitaani na kufunga barabara kuu huko nchini New Zealand na Australia.

Takriban watu 1,000 wamelifunga eneo la mzunguko wa taa za kuongozea magari la Grosser Stern, lililopo katika bustani ya Tiergarten katikati ya mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, katika maandamano yaliyoanza mapema jana.

Washirika wa vuguvugu hilo la Extinction Rebellion pia wametengeneza makambi nje ya ofisi ya kansela wa Ujerumani, Angela Merkel wakiwasilisha hoja yao ya kutoridhishwa na sera kuelekea mabadiliko ya tabia nchi iliyoandaliwa mwezi uliopita na serikali yake, kabla ya kuanza kwa maandamano hayo makubwa. Kulingana na vuguvugu hilo, maandamano hayo yatahusisha majiji 60 kote duniani.

Mjini Amsterdam, mamia ya waandamanaji wamezuia barabara kuu nje ya eneo maarufu kabisa la kitalii la Rijksmuseum, ambako pia wameweka mahema. Maandamano kwenye mji huo yaliendelea licha ya zuio la jiji. Wanaharakati hao walipuuzia miito ya polisi ya kuwataka kuondoka na kwenda kwenye bustani iliyo karibu na eneo walikokusanyika.

Mwanaharakati Elle van Zeeland ameliashibia shirika la utangazaji la Uholanzi NOS kwamba kundi hilo litaendelea kusalia hapo hadi serikali itakapokubaliana na madai yao. 

Neuseeland Extinction Rebellion Aktivisten in Wellington (Getty Images/H. Hopkins)

Mmoja ya wanaharakati wanaopigania hatua zaidi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huko New Zealand.

Wanaharakati hao wanataka serikali kusema ukweli kuhusu dharura ya mabadiliko ya tabianchi.

Huko nchini Australia, katika jiji la Sydney, polisi imesema inawashilikia waandamanaji 30 kwa madai ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kuzuia barabara na kupuuzia maelekezo kutoka kwa jeshi hilo.

Msemaji wa kundi hilo mjini Sydney Elly Baxter aliomba radhi kutokana na hatua hiyo ya kuzuia magari, lakini akasisitiza serikali imeshindwa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, "Tunaomba radhi kwa yoyote ambaye binafsi ameathiriwa na matendo yetu. hatutaki kuwa hapa. Hatutaki kutatiza maisha ya watu. Tunachotaka ni serikali kuchukua hatua. Tumejaribu sana kwa njia zetu ya kawaida lakini hazikufanikiwa. Kwa hiyo tunahisi tunasukumwa kuchukua hatua zisizo za kawaida".

Kundi hilo ambalo pia huitwa XR liliasisiwa nchini Uingereza mwaka jana na hadi sasa lina matawi kadhaa kwenye takriban mataifa 50.

Mkuu wa utumishi wa kansela Merkel Helge Braun amekosoa njia wanazotumia wanaharakati hao, na hususan za kufunga barabara kwa kuziita ni hatua hatari. Aidha amepuuzilia mbali hoja ya kutangaza suala la mazingira kuwa ni dharura akisema katiba hairuhusu kitu kama hicho. 

Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amesema maandamano ya aina hiyo hayawezi kuwakutanisha pamoja katika kutatua tatizo kwa kuzingatia kile wanachokihitaji.

 

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com