1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waamuzi wa kike Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza

18 Novemba 2022

Waamuzi wanawake watakaosimamia mechi kwa mara ya kwanza kabisa katika Kombe la Dunia, nchini Qatar wanasema wamechaguliwa sio tu kutokana na jinsia yao bali ueledi wao katika usimamizi wa mechi za kandanda.

https://p.dw.com/p/4Jkxr
Kombobild | Stephanie Frappart, Yoshimi Yamashita, Salima Mukansanga
Picha: Seskim Photo/IMAGO/AFLOSPORTS/IMAGO/Daniela Porcelli/SPP/IMAGO

Salima Mukansanga ni muamuzi wa mechi za kandanda anayetokea Rwanda na ni mmoja wa waamuzi watatu wa kati wa mechi, watakaosimamia mechi za Kombe la Dunia la mwaka huu.

Alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko mjini Doha Ijumaa, Mukansanga amesema,

"Tuko hapa kwasababu tunastahili kuwa hapa. Nyumbani katika mashirikisho yetu, huko ni kiwango tofauti cha kandanda ila hiki ndicho kiwango cha juu zaidi cha kandanda. Kwa hiyo uwepo wetu hapa unamaanisha tunastahili, si uamuzi uliochukuliwa tu kwa ajili ya kuleta mabadiliko au kwasababu tu sisi ni wanawake, la. Tumekuwa tukijituma na tunastahili, kwa hiyo tutaendelea kujituma na kuuonyesha ulimwengu kwamba tunastahili na tutashinda," alisema Mukansanga.

Qatar WM 2022 Schiedsrichterinnen
Muamuzi wa kutoka Rwanda Salima MukansangaPicha: Sebastian Frej/IMAGO

Waamuzi wengine wa kati wanawake waliochaguliwa ni Yamashita Yoshimi kutoka Japan na Stephanie Frappart ambaye ni raia wa Ufaransa.

Ronaldo kuwa mtu wa kwanza kufunga goli katika makombe matano ya dunia

Kwengineko mabingwa watetezi Ufaransa hawafahamu bado kama mshambuliaji wao Karim Benzema na beki Raphael Varane watakuwa imara kushiriki mechi yao ya ufunguzi Jumanne. Kiungo wa Les Bleus Adrien Rabiot alikuwa na haya ya kusema baada ya kuulizwa kuhusu hao wachezaji wenzake.

"Natumai Karim na Raphael wanaendelea vyema. Nina imani watakuwa na sisi karibuni, wanafany kila juhudi na naamini watakuwa nasi, hatuna shaka sana kuhusiana na hili," alisema Rabiot.

Hayo yakijiri Cristiano Ronaldo anatarajiwa kuwa mchezaji mwengine nyota kutua Qatar Ijumaa tayari kwa Kombe la Dunia.

Nyota huyo raia wa Ureno ambaye amekuwa kileleni mwa kandanda la dunia kwa kipindi cha miaka 15 pamoja na Lionel Messi wa Argentina atakuwa anashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tano na huenda hii ikawa mara yake ya mwisho kucheza katika mashindano hayo.

Ronaldo mwenye umri wa miaka 37 ameifungia timu yake ya taifa magoli 117 na analenga kuwa mchezaji wa kwanza duniani kufunga goli katika mashindano matano tofauti ya Kombe la Dunia aliyoshiriki. Ureno wako katika kundi moja na Ghana, Uruguay na Korea Kusini.

Fussball Sport l Auszeichnung l Spieler Cristiano Ronaldo
Nyota wa Ureno Cristiano RonaldoPicha: Patricia de Melo Moreira/AFP

Hakuna pombe katika viwanja vyote vya Kombe la Dunia

Wakati huo huo Shirikisho la Kandanda Duniani FIFA limetangaza kwamba hakutokuwa na uuzaji wa pombe katika viwanja vyote vitakavyochezewa mechi za Kombe la Dunia. FIFA imesema pombe zitauzwa tu katika maeneo yaliyo na vibali vya kuuza bidhaa hiyo.

Hatua hiyo imelaaniwa na Chama cha Mashabiki wa Kandanda kinachowakilisha mashabiki wa kandanda kutoka England na Wales, kilichosema kwamba hiyo ni ishara ya ukosefu wa mawasiliano kati ya waandaji wa mashindano hayo na mashabiki.

Pombe si marufuku Qatar ila inauzwa tu katika baa, migahawa na sehemu zilizo na vibali vya kuiuza. 

Chanzo: Reuters/AFP