1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya Ujerumani vyafanya vikao baada ya kuchaguliwa

John Juma
26 Septemba 2017

Wabunge wapya wa Ujerumani kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia wakutana Berlin huku vyama vingine pia vikifanya vikao. Wakati huo huo Merkel aweka mipango ya kufanya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano

https://p.dw.com/p/2kiMw
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Vyama vya kisiasa nchini Ujerumani vinafanya vikao vyao vya kwanza vya makundi ya bunge tofautitofauti. Mikutano hiyo ni ya kwanza tangu uchaguzi mkuu wa Jumapili ambapo chama cha Kansela Angela Merkel kilishinda japo kwa asilimia ndogo na sasa kinakabiliwa na changamoto ya kuunda serikali ya muungano kando na uwezekano wa kuwa na upinzani imara kutoka kwa vyama vya mirengo ya kulia na kushoto.

Wabunge wapya wa Ujerumani kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia - chama mbadala kwa Ujerumani AfD wanatarajiwa kufanya mkutano wao wa kwanza leo mjini Berlin tangu chama chao kiingie katika bunge la taifa. Mkutano huo wenye zaidi ya wajumbe 90 unajiri wakati wabunge wa vyama vingine pia wakitarajiwa kufanya vikao kutafakari mikakati yao katika bunge ambalo limekumbwa na mshtuko mkubwa.

Mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano

Wakuu wa vyama vya siasa wakishiriki kipindi cha televisheni baada ya uchaguzi kumalizika
Wakuu wa vyama vya siasa wakishiriki kipindi cha televisheni baada ya uchaguzi kumalizikaPicha: picture alliance/dpa/G. Breloer

Muungano wa Merkel wa vyama vya Christian Democratic Unioni CDU na Christian Social Union CSU, chama cha kijani, chama cha mrengo wa kushoto the Linke na washirika pia vinatarajiwa kukutana leo Jumanne.

Baada ya muungano wa CDU-CSU kupata ushindi uliopungua kwa asilimia 8.5, ikilinganishwa na uchaguzi mkuu miaka minne iliyopita, ushindi ambao unatajwa kuwa mbaya zaidi tangu mwaka 1949, Merkel sasa anakabiliwa na kibarua cha kujaribu kuunda serikali ya muungano. Merkel amesema anataka kuzungumza na vyama hivyo pamoja na SPD juu ya uwezekano wa kuwa washirika serikalini. Merkel amesema "Bila shaka nitataka kuzungumza na CSU na ninatumai tutapata suluhisho. Hakuna shaka, tutafanya kazi pamoja, pia nitatoa pendekezo kwa kiongozi wa sehemu nyingine na pia ninayo matumaini. Kwanza lazima kuwe na mazungumzo na hadi wakati huo kwa sasa siwezi kusema ikiwa yatafaulu au la."

Chama mshirika wa Merkel katika serikali ya sasa cha SPD kimeufuta uwezekano wa kushiriki tena katika serikali, na kusema kitakuwa katika upinzani. Hali hii inamuacha Merkel katika hali ngumu ya kujaribu kuunda serikali ya muungano ya vyama vitatu-chama chake CDU, FDP na chama cha Kijani.

Asilimia 57 wapendekeza muungano wa "Kijamaica"

Kansela Angela Merkel
Kansela Angela MerkelPicha: Reuters/F. Bensch

Kura ya maoni ambayo imetangazwa leo Jumanne na kituo cha televisheni ARD, imeonesha asilimia 57 ya wapiga kura wanaunga mkono serikali ya muungano itakayojumuisha CDU-CSU, kijani na FDP, maarufu "Jamaica" kutokana na rangi ya vyama hivyo kwa pamoja kufanana na bendera ya Jamaica.

Hata hivyo kiongozi wa chama cha kijani Cem Ozdemir tayari ameweka wazi msimamo wa chama chake kuelekea katika mazungumzo ya kuundwa serikali ya muungano. " Sharti la wazi la kufungua milango wazi kwa serikali ya muungano ni ulinzi wa mazingira. Hilo si suala la masihara ambalo tunalitumia kuwakasirisha watu, ni suala zito kwa mustakabali wa dunia yetu."

Kwa mara ya kwanza jumla ya vyama sita vilichaguliwa, kikiwemo  chama kinachotetea biashara FDP ambacho kilifanya kikao chake Jumatatu.

Mnamo Jumapili chama cha AfD kilikuwa chama cha kwanza cha siasa kali kuingia katika bunge tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia pale ilipopata asilimia 12.6 ya kura. Chama hicho kitakuwa cha tatu kwa ukubwa, nyuma ya CDU na SPD.

Mwandishi: John Juma/DPAE/APE

Mhariri:Iddi Ssessanga