Vita Iran yachochea mzozo wa mafuta usafiri wa ndege Afrika
22 Aprili 2026
Sekta ya usafiri wa anga duniani — ikiwemo ile inayokua kwa kasi barani Afrika — inakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi kutokana na athari za vita vya Iran.
Moja ya changamoto za papo hapo ni kupanda kwa gharama za mafuta ya ndege, ambayo huchangia sehemu kubwa ya gharama za uendeshaji wa mashirika ya ndege.
Mafuta ya ndege, ambayo ni aina ya mafuta ya taa (kerosene) yanayosafishwa kutoka mafuta ghafi, ndiyo hutumika kuendesha ndege.
Hata hivyo, usumbufu unaohusishwa na vita hivyo umefanya bei kupanda maradufu katika baadhi ya masoko, hali iliyosababisha pia upungufu wa bidhaa hiyo.
"Matokeo yake ni kwamba yameathiri kiasi cha mafuta ya ndege kinachonunuliwa na kampuni za usafiri wa anga barani Afrika kwa ajili ya shughuli zao,” amesema Dominick Andoh, mshirika mkuu wa AviationGhana, ambao ni mtandao wa habari za usafiri wa anga katika mazungumzo na DW.
Wasiwasi kuhusu usalama wa nishati umechangia kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Katika biashara za mapema siku ya Jumatano, mafuta ghafi ya Brent yalikuwa yakikaribia dola 98 kwa pipa — yakiongezeka kwa zaidi ya asilimia 30 tangu kuanza kwa vita, kwa mujibu wa Reuters.
Wachambuzi wanaeleza kuwa ongezeko hilo linatokana na hofu kwamba makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran yanaweza kuvunjika, hasa baada ya Marekani kukamata meli ya mizigo ya Iran na usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz kuendelea kusimama kwa kiasi kikubwa.
Mtaalamu Dominick Andoh ameongeza kuwa ongezeko hilo la bei za mafuta limehamishiwa kwa abiria. "Bei za tiketi zimeongezeka,” alisema.
"Ukiangalia gharama za ziada za mafuta (fuel surcharge) kwenye tiketi nyingi zilizouzwa tangu vita kuanza, hasa mwezi Aprili, zimeongezeka kwa viwango tofauti.”
Usumbufu wa safari za ndege waongeza hasara za kifedha
Ukubwa wa mgogoro huu umeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa viongozi wa biashara barani Afrika.
"Mashirika mengi ya ndege barani Afrika hayataweza kuhimili” ongezeko la sasa la gharama za mafuta, amesema bilionea wa Nigeria Aliko Dangote, mmiliki wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote kilicho karibu na Lagos, akizungumza katika mkutano wa uchumi wa dunia wa Semafor uliofanyika Washington, D.C.
Mbali na gharama za mafuta, vizuizi vya anga katika nchi za Ghuba vimezilazimisha kampuni za ndege kubadili njia au kufuta safari, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji na kupunguza ufanisi wa safari. Usumbufu huo pia umechangia kupanda kwa bei za tiketi.
Ethiopian Airlines ni miongoni mwa mashirika yaliyoathirika zaidi. Mwezi uliopita, maafisa wa shirika hilo walieleza kuwa linapoteza takribani dola milioni 137 kila wiki kutokana na mgogoro huo.
Meneja wa biashara wa shirika hilo, Lemma Yadhecha, alisema kuwa zaidi ya safari 100 kwa wiki zimefutwa, huku baadhi ya njia zilizokuwa zikihudumiwa mara tatu kwa siku zikiathirika vibaya.
Tangazo la kusitisha mapigano lililotolewa wiki iliyopita lilitoa matumaini ya muda mfupi kwa sekta ya anga, lakini matumaini hayo yalipungua haraka kutokana na hofu kuwa makubaliano hayo yanaweza kuvunjika wakati wowote.
Mashirika yabuni mikakati mipya kuendelea kujiendesha
Kutokana na changamoto zinazoongezeka, baadhi ya mashirika ya ndege barani Afrika yameanza kutumia mikakati mbadala ili kuendelea na shughuli zao.
Kwa mfano, Kenya Airways imesema imeanza kuwaelekeza wasafiri wengi wa Ulaya kupitia kitovu chake cha Nairobi badala ya kutumia njia za kawaida kupitia nchi za Ghuba.
"Tumechukua fursa ya hali ya sasa na kuelekeza wateja wengi kutoka Ulaya kupitia Kenya, badala ya kupita katika maeneo ya Ghuba,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, George Kamal.
Licha ya changamoto hizo, mtaalamu Dominick Andoh anaamini kuwa sekta ya usafiri wa anga barani Afrika inaweza kuhimili hali hiyo ikiwa mashirika yatachukua hatua za tahadhari.
Amesema mashirika yanaweza kuongeza akiba ya mafuta ya ndege pale inapowezekana, pamoja na kujikinga dhidi ya mabadiliko ya bei (hedging) ili kupunguza athari iwapo vita vitaendelea kwa muda mrefu.
Hata hivyo, mkuu wa Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga, Willie Walsh, ameonya kuwa hata kama Mlango wa Hormuz utafunguliwa tena, itachukua miezi kadhaa kurejesha usambazaji wa mafuta katika kiwango cha kawaida.
Amesema usumbufu katika uwezo wa kusafisha mafuta Mashariki ya Kati — eneo muhimu kwa usambazaji wa bidhaa za mafuta duniani — utaendelea kuathiri si tu mafuta ya ndege bali pia bidhaa nyingine, na hivyo kuchelewesha kurejea kwa hali ya kawaida.
Sekta ya utalii nayo yaathirika
Mgogoro wa usafiri wa anga umeathiri pia sekta ya utalii, ambayo inategemea kwa kiasi kikubwa usafiri wa ndege.
Nchini Afrika Kusini, waendeshaji wa utalii kama Emraan Roode kutoka Cape Town wanasema kufutwa kwa safari na hali ya kutokuwa na uhakika tayari vinaathiri maisha yao.
"Cape Town ni moja ya maeneo bora duniani kwa watalii, lakini kutokana na vita, sekta ya utalii imeathirika kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na waongoza watalii na makampuni ya utalii,” amesema Roode akizungumza na Reuters.
Kufutwa kwa safari, hasa zile zinazohusiana na njia za Mashariki ya Kati, pia kumeathiri biashara zinazotegemea wateja wa kimataifa wanaorudi mara kwa mara.
Amesema amepoteza kati ya randi 350,000 hadi 500,000 (sawa na dola 21,000 hadi 30,000) katika miezi ya karibuni kutokana na vita vya Mashariki ya Kati, hali iliyopunguza idadi ya wateja waliokuwa wakirudi mara kwa mara.
Hata hivyo, mtaalamu Dominick Andoh anaendelea kuwa na matumaini kuwa sekta za anga na utalii zitarejea katika hali ya kawaida.
"Sekta ya anga na utalii zitaendelea kuwepo. Kama ilivyoonekana wakati wa janga la COVID-19, sekta hizi zina uwezo mkubwa wa kuhimili misukosuko. Watu wataendelea kusafiri,” amesema.