Viongozi wa Syria na Urusi wakutana | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Syria na Urusi wakutana

Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil yuko nchini Urusi kwa mazungumzo na waziri wa mambo ya nchi za nje juu ya namna ya kumaliza mgogoro wa Syria, uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil

Naibu Waziri Mkuu wa Syria Qadri Jamil

Kulingana na afisaa mkuu wa Syria, Urusi na Syria zitazungumzia pia uwezekano wa Urusi kutoa msaada wa kifedha kwa Syria kusaidia kuukwamua uchumi wake uliosambaratika kutokana na vita vinavyoendelea.

Naibu waziri mkuu huyo Qadri Jamil amesema jambo hilo limezungumziwa na wanatumai kupata jibu kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mwanajeshi wa Syria

Mwanajeshi wa Syria

Jamil amesema kwa sasa ni mapema sana kujua ni kiwango gani cha fedha watakachopokea. Kando na hilo Syria imesema mpango wa kutatanisha wa Urusi kupeleka mfumo wa makombora aina ya S-300 nchini humo bado inazingatiwa.

Wakati huo huo shirika la habari la kitaifa nchini Urusi la Interfax limesema pande zote mbili ziliamua mwezi uliopita katika mkutano uliofanyika kaskazini mwa Ireland kwamba watafanya kazi pamoja ili kuwaondoa magaidi na makundi yalio na itikadi kali nchini Syria.

Sergei Lavrov asema upinzani hauna nia ya mazungumzo

Hii leo Waziri wa Mambo ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema upinzani bado haujaonesha nia ya kujiunga na mazungumzo hayo.

Waziri wa Mambo ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov

Waziri wa Mambo ya nchi za kigeni wa Urusi Sergei Lavrov

"Tunaendelea kukutana na serikali na makundi yote ya upinzani kuwashawishi wote kwamba ni muhimu kujiunga na mchakato huu wa amani haraka iwezekanavyo," Alisema Sergei Lavrov.

Waziri huyo amesema pia kwa sasa idadi kubwa ya upinzani haijaonesha nia ya kujiunga na mazungumzo.

Hata hivyo ziara ya Naibu waziri mkuu wa Syria Qadri Jamil nchini Urusi imekuja baada ya Ahmad al-Jarba, mkuu wa muungano wa upinzani nchini Syria kukutana na viongozi wa Misri na Saudia wikendi iliopita, kabla ya kuelekea Ufaransa kukutana kwa mazungumzo na rais wa nchi hiyo Francois Hollande.

Mashambulizi zaidi Syria

Huku hayo yakiarifiwa wanaharakati wa Syria wamesema waasi 75 wameuwawa kwenye makabiliano na vikosi vya serikali saa 24 zilizopita katika kung'ang'ania udhibiti wa mji mkuu Damascus.

Ahmad Al-Jarba na Waziri wa mambo ya Kigeni wa Misri Nabil Fahmi

Ahmad Al-Jarba na Waziri wa mambo ya Kigeni wa Misri Nabil Fahmi

Idadi nyengine ya vifo ilioripotiwa na shirika la kutetea haki za binaadamu lililo na makao yake mjini London,Uingereza inajumuisha waasi 49 waliouwawa katika shambulizi la Kaskazini Mashariki mwa mji wa Adra mapema jana asubuhi.

Shirika hilo limesema vikosi vilivyotiifu kwa Rais Bashar Al Assad viliwavamia waasi hao walipokuwa wanajaribu kuingia mjini humo.

Hata hivyo shirika la habari la taifa nchini Syria SANA liliripoti mashambulizi hayo bila kutoa idadi ya waliojeruhiwa.

Kwa sasa Shirika la Umoja wa Mataifa linakadiria watu takriban elfu 93,000 wameuwawa tangu kuanza kwa machafuko nchini Syria zaidi ya miaka miwili iliopita.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa/AFP/AP

Mhariri: Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com