1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa nchi wakutana katika mkutano wa kilele wa APEC

10 Novemba 2014

Viongozi wa China na Japan wamefanya mkutano wa nadra baina yao hii leo baada ya miaka miwili ya uhasama kati ya nchi zao. Mazungumzo yao yanafanyika pembezoni mwa mkutano wa kilele wa nchi za Asia na Pacifiki APEC

https://p.dw.com/p/1Djqu
Picha: Reuters/Kevin Lamarque

Rais wa China Xi Jinping na Waziri mkuu wa Japan wamekutana katika kile ambacho Abe amekitaja kuwa hatua ya kwanza katika kurekebisha uhusiano uliovunjika kati ya nchi hizo mbili zenye nguvu za kiuchumi.

China ambayo ni ya pili kwa uchumi imara duniani, na Japan ambayo iko katika nafasi ya tatu, zimekuwa zikizozana vikali kwa miaka miwli iliyopita kuhusu visiwa, ubabe wa kikanda na suala la tangu jadi kuhusu vita kati ya nchi hizo mbili ambavyo Japan iliikalia China.

China na Japan kuboresha uhusiano

Mkutano kati ya viongozi hao unakuja baada ya wanadiplomasia wakuu wa nchi zao kukubaliana wiki iliyopita kuboresha uhusiano na kuweka kando tofauti kati yao.Abe amesema wamekutana wakiwa na lengo la kuanza kushughulikia tofauti zilizopo.

Rais wa China Xi Jinping na waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe
Rais wa China Xi Jinping na waziri mkuu wa Japan Shinzo AbePicha: Reuters/Kim Kyung-Hoon

Rais wa Marekani Barrack Obama naye amewasili nchini China hii leo kuhudhuria mkutano wa kilele wa jumuiya ya ushirikiano wa nchi za Asia na Pacific APEC ambao pia unahudhuriwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye nchi yake na Marekani zimeshuhudia uhusama baridi katika miezi ya hivi karibuni.

Obama ambaye yuko katika ziara ya siku nane barani Asia na Pacific amesema anaona kasi ikizidi katika kuafikiwa kwa makubaliano ya kuwepo biashara huru ya mpango unaopendekezwa na nchi yake utakaozihusisha nchi 12 tu kati ya nchi wanachama 21 wa APEC ujulikanao TPP.

Masuala ya kisiasa pia yatajadiliwa

Mkutano huo wa APEC ndiyo mkubwa kabisa kuwahi kuandaliwa na rais wa China tangu achukue madaraka mwaka jana na unawaleta pamoja viongozi wa baadhi ya nchi kubwa kiuchumi duniani kwa siku mbili zijazo wakiwa na lengo la kuboresha uhusiano wa kibiashara kati yao na pembezoni mwa mkutano huo wakijaribu kushughulikia masuala ya siasa za udhibiti wa kanda.

Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa China Xi Jinping katika mkutano wa APEC
Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa China Xi Jinping katika mkutano wa APECPicha: picture-alliance/dpa/EPA/HOW HWEE YOUNG

China na Marekani zinatarajiwa kila mmoja kusukuma ajenda tofauti za kufikiwa kwa makubaliano ya kibiashara ambayo hayahusishi upande mwingine.Mkutano wa APEC utapiga darubini ushindani uliopo kati ya nchi kubwa zilizostawi kiuchumi Marekani, China na Urusi.

Putin na Xi walikutana hapo jana ambapo kiongozi wa China alimuambia Putin kuwa aendelee kuvuna matunda ya urafiki wao. Xi alimuambia Putin kuwa licha ya mambo katika ulingo wa kimataifa kuonekana kubadilika wanapaswa kusalia katika njia waliyoichagua ya kutanua na kuimarisha ushirikiano mzuri kati yao.

Mkutano huo wa APEC unafungua wiki ya mikutano mingine ya ngazi ya juu ambapo baada ya Beijing, viongozi wanatarajiwa kuelekea Myanmar kwa mkutano wa kilele wa kiuchumi wa nchi za mashariki mwa Asia na kufuatiwa na mazungumzo ya nchi ishirini zenye nguvu zaidi za kiuchumi duniani G20 utakaofanyika mjini Brisbane,Australia.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel