1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa eneo la Maziwa Makuu waijadili Congo

Admin.WagnerD9 Oktoba 2018

Marais na viongozi wa kanda ya maziwa makuu waliosaini mkataba wa amani, usalama na ushirikiano na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wamekamilisha mkutano wao mjini Kampala, Uganda.

https://p.dw.com/p/36EAh
Yoweri Museveni Präsident Uganda
Picha: Getty Images/AFP/G. Grilhot

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa asubuhi ya leo baada ya mkutano huo jana jioni, viongozi hao wameazimia kuendelea kuushawishi utawala wa rais wa Congo, Joseph Kabila, kuimarisha juhudi za kukomesha vitendo vya kigaidi na mateso kwa binadamu hasa katika eneo la Mashariki mwa Congo.

Kwa mujibu wa azimio lao la kukomesha mizozo na mateso kwa raia katika eneo la maziwa makuu hasa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, viongozi na wajumbe wa ngazi za juu kutoka mataifa 11 walikuwa  na  mkutano wao wa awamu ya tisa chini ya mkataba wa muundo wa amani, usalama na ushirikiano uliosainiwa mwezi Februari mwaka 2013. Chini ya mkataba huo nchi hizo zilizo na mipaka na Congo  zinatarajiwa kuisaidia nchi hiyo  kuleta amani ndani ya nchi, jambo ambalo litachangia katika kuimarisha amani katika kanda hiyo ya maziwa makuu. Rais Museveni  amekabidhiwa Uwenyekiti wa jopo hilo.

Madini chanzo cha mzozo Congo

Hivi karibuni kumekuwepo na mjadala kuwa mizozo, vita na ukiukaji wa haki za binadamu hasa mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kunatokana utajiri mkubwa wa madini. Biashara haramu za madini hayo ikitajwa kuwa chanzo cha mapato kwa makundi ya waasi na hata kuhusishwa wanajeshi wa kulinda amani wa umoja mataifa.

Edgar Lungu Zambia Präsident
Rais Edgar Lungu wa ZambiaPicha: picture-alliance/P.Wojazer

Rais wa Zambia, Edgar Lungu, ambaye aliongoza ujumbe wa Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika, SADC, alirudia wito kwa kuwataka wadau wote kukabiliana na hali hiyo.

Ikumbukwe kuwa makundi mbalimbali ya waasi dhidi ya tawala za Rwanda, Uganda na hata Jamhuri ya Kidemokrasi ya  Congo yenyewe yanaendelea na harakati zao katika sehemu hiyo. Kwa sasa kuzuka kwa janga la ebola kumesababisha  hofu mpya kutokana na ukosefu wa uthabiti katika eneo hilo, hali inayosababisha matatizo makubwa kwa  watalamu wa tiba kuudhibiiti ugonjwa huo.

Mkutano huo uliohudhuriwa pia  na wawakilishi kutoka Umoja mataifa, Umoja wa Afrika na mashirikisho ya kibiashara umeorodhesha maazimio kadhaa ili  kufanikisha juhudi za kuleta amani na usalama nchini Congo.

Lubega Emmanuel DW Kampala.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman