1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa DRC hawataki wasimamizi wa Uchaguzi

Oumilkheir Hamidou
24 Agosti 2018

Vizingiti vya kila aina vinaizonga jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo miezi minne tu kabla ya uchaguzi utakaoamua hatima ya nchi hiyo ambayo ni mojawapo ya nchi zinazozongwa na mizozo ya kila aina ulimwenguni..

https://p.dw.com/p/33gay
DRC Präsident Joseph Kabila
Picha: picture-alliance/AP/J. Bompengo

Umoja wa Mataifa, Afrika Kusini, Umoja wa ulaya na wengineo, wote hao jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, inasema haihitaji msaada wao, washauri wao wala maoni yao kuhusu maandalizi ya uchaguzi uliopangawa kuitishwa Desemba 23 inayokuja.

Kinshasa inataka kuwaweka kando "wajumbe maalum" na wasimamizi wengineo, na zoezi la uchaguzi ambalo lengo lake kuu ni kupatikana kwa mara ya kwanza kipindi  cha mpito kwa njia ya amani nchcini humo.

Hadi wakati huu ratiba inaheshimiwa tangu rais Joseph Kabila aliposema hatogombea tena na badala yake kumteuwa "mfuasi wake". Orodha ya muda ya wagombea inatarajiwa kutangazwa wakati wowote hii leo.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki (kati kati) akiwi na wasimamizi wengine wa uchaguzi Agosti mwaka 2017 mjini Nairobi Kenya.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki (kati kati) akiwi na wasimamizi wengine wa uchaguzi Agosti mwaka 2017 mjini Nairobi Kenya.Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

 Rais wa zamani wa Afrika Kusini pia hatakiwi

Jumatatu iliyopita viongozi wa mjini Kinshasa walipinga ripoti iliyotangazwa na vyombo vya habari, bila ya kuthibitishwa na serikali kuhusu kuteuliwa rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki kuwa "mjumbe maalum" katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

"Nnaweza kukwambieni, hakutokuwepo tena na mjumbe maalum yeyote katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo, hata kama ni Thabo Mbeki" alisema mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa rais Kabila, Barnabé Kikaya Bin Karubi.

Anawalaumu  wajumbe hao  na kudai wana mtindo wa kujigeuza "mabalozi wadogo", hawaheshimu mamlaka ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo."Tunataka kudhihirisha tuko huru", amesema kwa upande wake waziri wa mawasiliano Lambert Mende.

Mtambo wa Computor ambao wapiga kura watalazimika kuutumia kwa mara ya kwanza kutoa sauti zao
Mtambo wa Computor ambao wapiga kura watalazimika kuutumia kwa mara ya kwanza kutoa sauti zaoPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Viongozi wa Kinshasa wanataka kuficha ukweli wa mambo

Msimamo wa serikali ya Kinshasa dhidi ya wasimamizi wa Umoja wa mataifa, Umoja wa Ulaya na Afrika Kusini unaangaliwa kwa jicho la wasi wasi na wadadisi. Mtaalam wa masuala ya katiba  kutoka mashirika ya kiraia André Mbata Mangu anasema tunanukuu" kuukataa ujumbe wa Thabo Mbeki ni dalili kwamba  jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo  inataka kuficha mambo mengi yasigunduliwe na jumuia ya kimataifa."

Siku chache kabla tume ya uchaguzi ilisema haihitaji ndege na helikopta za tume ya umoja wa Mataifa nchini Kongo-MONUSCO ili kusafirisha zana za uchaguzi katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba milioni mbili na laki nane na wapiga kura milioni 40 waliosajiliwa.

"Hatulazimishi" walijibu wakati ule maafisa wa tume ya Mosnuco."

Serikali ya mjini Kinshasa inapendelea kuwaona wanajeshi wa tume ya kulinda amani wa umoja wa mataifa-MONUSCO wakiihama nchi hiyo hadi ifikapo mwaka 2020.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga