1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi duniani wampongeza Waziri Mkuu mpya wa Israel

14 Juni 2021

Viongozi mbalimbali duniani wamemtumia salamu za pongezi waziri mkuu mpya wa Israel Naftali Bennett aliyechukua wadhifa huo baada ya Bunge la nchi hiyo kuidhinisha serikali mpya ya mseto ya vyama vya upinzani.

https://p.dw.com/p/3uqW6
Israel Naftali Bennett Politiker
Naftali Bennett, waziri mkuu mpya wa IsraelPicha: Menahem Kahana/AFP/Getty Images

Salamu hizo za pongezi zinafuatia ushindi mwembamba uliopatikana katika bunge la Israel siku ya Jumapili ambao umemwezesha Naftali Bennett, mwanasiasa kutoka chama kidogo cha Yamina, kuchukua wadhifa wa waziri mkuu chini ya serikali ya mseto ya vyama nane vya siasa na kumaliza enzi ya uongozi wa Benjamin Netanyahu. 

Serikali ya Bennet imeidhinishwa kwa ushindi wa kura moja tu baada ya kuridhiwa na wabunge 60 huku ikipingwa na wabunge 59 katika bunge lenye viti 120. Inaarifiwa mbunge mmoja alijizuia kupiga kura.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amempongeza Bennet kwa kuapishwa kuiongoza Israel na kumuahidi kuwa serikali yake itafanya naye kazi katika suala la usalama wa Israel na kutafuta amani kwenye kanda ya Mashariki ya Kati.

Salamu sawa na hizo zimetolewa na rais Joe Biden wa Marekani ambaye amesema Washington inasalia kuwa mshirika mkuu na muhimu wa Israel na itaendelea kuiunga bila kutetereka.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya, Charles Michel, Kansela Sebastian Kurz  wa Austria na mawaziri wakuu wa Uingereza na Canada nao pia wamepongeza Bennet kwa ushindi aloupata Bungeni na kuwa waziri mkuu.

Hamas wasema mapambano yanaendelea 

Hata hivyo kundi la wapiganaji wa Hamas linaloongoza Ukanda wa Gaza ambalo ni hasimu wa Israel lenyewe halikutuma ujumbe wa pongezi na badala yake limesema mapambano dhidi ya Israel yataendelea bila kujali nani anaongoza serikali.

Jair Lapid
Yair Lapid, kiongozi wa chama cha Yesh AtidPicha: Debbie Hill/AP Photo/picture alliance

Kwa upande wake serikali ya mamlaka ya ndani ya Palestina iliyo na nguvu upande wa Ukingo wa Magharibi imeyakaribisha mabadiliko ya uongozi mjini Tel Aviv lakini imesema kipaumbele chake ni kuundwa kwa taifa huru la Palestina chini ya mipaka iliyokuwepo kabla ya vita vya mwaka 1967.

Bennett, ambaye ni waziri wa ulinzi wa zamani na mshirika wa wakati fulani wa Benjamin Netanyahu atashika wadhifa wa waziri mkuu kwa muda wa miaka miwili na kisha kumkabidhi wadhifa huo Yair Lapid, kiongozi wa chama cha Yesh Atid kilicho sehemu ya muungano wa upinzani.

Bennett aonya kuhusu Iran na kulitahadharisha kundi la Hamas

Israel Knesset | Netanjahu und Bennett
Benjamin Netanyahu (kushoto) akimpongeza waziri mkuu mpya Naftali BennettPicha: Ronen Zvulun/REUTERS

Katika hotuba yake aliyoitoa kabla ya kura Bungeni, Bennett alizungumzia masuala kadhaa ya kisera ikiwemo upinzani wake kwenye mpango unaoendelea wa kuufufua mkataba wa nyuklia kati ya Iran na madola yenye nguvu.

Kiongozi huyo amesema Israel haitaruhusu Iran itengeneza silaha za nyuklia.

Kadhalika amelionya kundi la Hamas kuwa litakabiliana na "mkono wa chuma" iwapo litafanya tena mashambulizi ya maroketi dhidi ya Israel.

Ushindi wa Bennett na muungano wa upinzani ulipokelewa kwa kishindo mjini Tel Aviv ambako watu walimiminika mitaani kushangilia huku wakipeperusha bendera za Israel na kupiga honi za magari.