Varoufakis ajiuzulu wadhifa wa waziri wa fedha | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Varoufakis ajiuzulu wadhifa wa waziri wa fedha

Waziri wa Fedha wa Ugiriki Yanis Varoufakis amejiuzulu katika kile kinachoonekana kuwa ni mwafaka wa Waziri Mkuu Tsipras na wakopeshaji wake baada ya kupata ushindi mkubwa katika kura ya maoni kuhusu mpango wa mkopo

Tangazo hilo la kushangaza lililofanywa na Varoufakis limekuja wakati viongozi wa UIaya wakiendelea kutafuta jibu baada ya wapiga kura wa Ugiriki kusema kwa wingi “hapana” kwa hatua zaidi za kubana matumizi zilizoitishwa na wakopeshaji ili nchi hiyo ipewe fedha za mkopo, katika kura ya maoni ambayo huenda ikaifanya nchi hiyo kuondoka katika kanda ya sarafu ya euro.

Varoufakis ambaye amewahi kupambana na wakopeshaji katika miezi iliyopita, amesema anajiuzulu wadhifa huo kwa sababu lilikuwa wazo ambalo Waziri Mkuu alihisi kuwa lingemsaidia kufikia makubaliano na wakopeshaji.

Safaru ya euro iliimarika thamani baada ya tangazo la Varoufakis, ambalo lilitarajiwa kuimarisha matumaini kuwa wakopeshaji wa Ugiriki – Benki Kuu ya Ulaya, Halmashauri Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF – huenda wakashawishiwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo licha ya uamuzi wa Ugiriki wa kupinga masharti ya mageuzi waliyoyaitisha kabla ya kutoa fungu la mwisho la fedha za mkopo.

Griechenland Referendum Tsipras TV

Waziri Mkuu wa Ugiriki Tsipras aliwahutubia wananchi akiwapongeza kwa maamuzi yao

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitarajiwa kukutana na Rais wa Ufaransa Francois Hollande mjini Paris pamoja na mikutano mingine ili kutafakari athari za kura hiyo, ambayo ilikuwa ushindi kwa chama cha siasa za mrengo wa kushoto cha Tsipras, ambaye alisisitiza kuwa haikulenga kuipasua Ulaya.

Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema mkutano wa kilele wa dharura wa kanda ya sarafu ya euro utaandaliwa kesho. Wakati wachambuzi wakisema kuna uwezekano mkubwa wa Ugiriki kiondoka katika kanda ya euro, mkuu wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker alitarajiwa kufanya mazungumzo na mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi, Tusk, na mkuu wa kundi la mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya Jeroen Dijsselbloem.

Wakati huo huo, mawaziri wa fedha wa Ujerumani na Ufaransa wanatarajiwa kufanya mazungumzo kuanzia mjini Warsaw wakati maafisa wakuu wa fedha wa kundi la sarafu ya euro wakikutana mjini Brussels.

Viongozi wa UIaya wametoa hisia tofauti kutokana na takwimu zilizotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya Ugiriki mapema leo zikionyesha matokeo ya mwisho ya kura ya maoni kuwa asilimia 61.31 walipiga kura ya “Hapana” na asilimia 38.69 wakasema “Ndiyo”. Asilimia 62.5 ilishiriki katika upigaji kura huo.

Waziri wa Uchumi wa Ujerumani ambaye pia ni naibu kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel ameliambia gazeti la Tagespiegiel kuwa Tsipras amevunja madaraja kati ya Ugiriki na Ulaya. Amesema licha ya matamshi ya Tsipras, mazungumzo mapya ya fedha za mkopo sasa ni magumu kufikiria. Uingereza imeapa kufanya kila iwezalo kuulinda usalama wa uchumi wake kutokana na kura hiyo ya Ugiriki.

Maelfu ya watu walikusanyika mjini Athens jana usiku kushangilia ushindi wa “Hapana“.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com