1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiKimataifa

Oxfam: Utajiri wa mabilionea wapanda kwa 20% tangu 2020

19 Januari 2026

Idadi ya mabilionea duniani inaendelea kuongezeka, na utajiri wao unaongezeka kwa kasi, kulingana na ripoti iliyochapishwa na shirika la Oxfam kabla ya kuanza kwa Jukwaa la Uchumi Duniani huko Davos Jumatatu.

https://p.dw.com/p/574PJ
Marekani Glendale 2025 | Ibada ya kumuaga mchambuzi wa kihafidhina aliyeuawa Charlie Kirk
Mtu tajiri zaidi duniani Elon Musk akipunga mkono katika shughuli ya kumuaga aliyekuwa mtangazaji Charlie Kir, Arizona, Marekani. Septemba 21, 2025 Picha: Daniel Cole/REUTERS

Shirika hilo la Oxfam linalopambana na umaskini na kushughulika na masuala ya maendeleo, ambalo hutoa ripoti ya kila mwaka kuhusu ukosefu wa usawa duniani kabla ya mkutano wa Davos, lilisema takriban mabilionea 3,000 duniani walikuwa na utajiri wa jumla wa dola trilioni 18.3 mwaka jana.

Licha ya kutetereshwa na mfumuko wa bei, utajiri wao umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 tangu Machi 2020. Wakati huo huo, karibu nusu ya idadi ya watu duniani wanaendelea kuishi katika umaskini Oxfam ilisema.

Ripoti hiyo inatokana na takwimu kutoka vyanzo vingi, ikiwa ni pamoja na makadirio ya jarida la Forbes kuhusu utajiri wa mabilionea, takwimu za Benki ya Dunia na Ripoti ya Utajiri ya Kimataifa ya UBS.

Kenya Turkana 2011 | Watu wakisubiri msaada wa chakula kutoka Oxfam
30.08.2011 *** Watu wa Turkana wakisubiri kwenye foleni kupokea chakula kutoka Oxfam katika wilaya ya kati ya Turkana, Kenya.Picha: Tobin Jones/AP Photo/picture alliance

Watu 12 ni matajiri kuliko zaidi ya watu bil. 4 duniani

Utajiri wa mabilionea ulikua kwa takriban asilimia 16 mwaka jana - mara tatu zaidi kuliko miaka iliyopita, kulingana na Oxfam. Watu 12 matajiri zaidi duniani sasa wana utajiri zaidi kuliko nusu ya watu maskini zaidi duniani, ambao ni zaidi ya watu bilioni nne.

Mtu tajiri zaidi duniani, Elon Musk, kwa kila sekunde nne hupata kile ambacho mtu wa kawaida hukipata kwa mwaka, Oxfam ilisema. Ilihesabu kwamba Musk angehitaji kutoa zaidi ya dola 4,500 kwa kila sekunde ili utajiri wake uanze kupungua.

Ulinganisho mwingine wa utajiri kulingana na Oxfam unaonyesha: - Watu wanne matajiri zaidi duniani wana thamani ya zaidi ya ng'ombe wote duniani.

Marekani Washington 2025 | Trump na Elon Musk katikati ya mgawanyiko wa kisiasa kabla ya kuondoka kwenda Mar-a-Lago
Rais wa Marekani Donald Trump na Elon Musk (Kulia) wakizungumza kabla ya kuondoka Ikulu ya White House akielekea nyumbani kwake South Florida huko Mar-a-Lago huko Florida mnamo Machi 14, 2025.Picha: Roberto Schmidt/AFP

Takriban viongozi 65 wa dunia wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano wa jukwaa la mwaka huu huko Davos, Uswisi - idadi kubwa zaidi - pamoja na wakuu kadhaa wa Benki Kuu na mawaziri wa fedha, pamoja na viongozi wa kibiashara duniani.

Wasiwasi kuhusu mamlaka ya kisiasa

Oxfam pia ilionya kwamba ushawishi unaoongezeka sana wa kiuchumi miongoni mwa mabilionea unazidi kubadilika na kuwa ushawishi wa kisiasa, hasa nchini Marekani, jambo ambalo ilisema linaharibu mifumo ya kidemokrasia.

Ripoti hiyo pia iliibua wasiwasi kuhusu mkusanyiko wa vyombo vya habari duniani, ikiandika kwamba "zaidi ya nusu ya makampuni makubwa ya vyombo vya habari duniani yanamilikiwa na mabilionea na makampuni tisa kati ya 10 bora ya mitandao ya kijamii duniani yanaendeshwa na mabilionea sita tu."