1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiKimataifa

Ujerumani yakubali kutoa akiba ya mafuta kulinusuru soko

11 Machi 2026

Ujerumani na Austria tayari wamesema wataruhusu sehemu ya akiba yao ya mafuta kutumika kufuatia ombi la Shirika la Nishati la Kimataifa IEA kwa wanachama wake kutoa mapipa milioni 400.

https://p.dw.com/p/5ABLQ
Marekani Chicago 2026 | Bei za mafuta kama zinavyoonekana zimepanda baada kutokana na vita na Iran
Shirika la Nishati la Kimataifa, IEA limewaomba wanachama wake kutoa mapipa milioni 400 ili kupambana na kadhia ya kupanda kwa bei ya nishatiPicha: Scott Olson/Getty Images/AFP

Lengo la ombi la Shirika la IEA ni kupambana na kadhia ya kupanda kwa bei ya nishati kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na baada ya wawaziri wa nishati wa mataifa hayo kusema wako tayari kuchukua hatua zote muhimu.

Waziri wa nishati wa Ujerumani Katherina Reiche amesema Ujerumani iko tayari kukubaliana na ombi hilo ikiwa litapitishwa, licha ya kwamba bado iko salama katika eneo la ugavi wa mafuta

Aliongeza "Shirika la Nishati la Kimataifa liliziomba nchi wanachama wake jana jioni kutoa akiba ya mafuta inayofikia mapipa milioni 400, au tani milioni 54 nzuri. Tutazingatia ombi hili na kutoa mchango wetu. Hii ni kwa sababu Ujerumani inaunga mkono kanuni muhimu zaidi ya IEA ya mshikamano wa pande zote. Ikiwa pendekezo hilo litakubaliwa, Wizara ya Uchumi ya Ujerumani itaingia mara moja katika mazungumzo na Jumuiya ya Wasambazaji Petroli ili kufafanua kwa undani kuhusu kutolewa kwa akiba ya Ujerumani."

IEA | Shirika la Kimataifa la Nishati
Shirika la Nishati la Kimataifa la IEA lawaomba wanachama wake kutoa mapipa milioni 400 ili kupambana na kadhia ya kupanda kwa bei ya nishatiPicha: rafapress/Zoonar/IMAGO

Mataifa ya G7 yatangaza utayari wa kutoa mafuta ya akiba

Mataifa saba yenye nguvu kiuchumi ulimwenguni G7 yametangaza hii leo kuwa yako tayari kutumia akiba ya kimkakati ya mafuta ili kukabiliana na ongezeko la kupanda kwa bei ya mafuta ghafi kutokana na vita hivyo kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati.

Ni tangazo lililotolewa katika mkutano kwa njia ya video ulioongozwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, mjini Paris, kabla wakuu wa mataifa hayo ya G7 hawajakutana kujadiliana kuhusu kuporomoka kwa uchumi kunakoshuhudiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na vita hivyo vya Marekani na Israel dhidi Iran ambavyo vimeingia wiki ya pili.

Mawaziri hao wa nishati wamesema kimsingi, wanaunga mkono utekelezaji wa hatua za haraka za kushughulikia hali hiyo, ikiwa ni pamoja na matumizi ya akiba ya kimkakati. Ufaransa kwa sasa ndio rais wa mzunguko wa IEA.

Jana Jumanne, mataifa wanachama wa lenye makao yake mjini Paris yalifanya mazungumzo kuangazia mzozo huo, ili kutathmini usalama wa usambazaji na uwezekano wa kutolewa kwa akiba ya dharura wakati mzozo huo ukiendelea kuathiri masoko. Japan nayo imesema itaruhusu kiasi cha mafuta yake ya akiba kuanzia Jumatatu.

Mataifa yazidi kupambana kutafuta suluhu

Soko la mafuta ghafi limeathirika pakubwa tangu Marekani na Israel zilipoanza kuishambulia Iran mwishoni mwa mwezi uliopita, huku Tehran ikilipiza kisasi kwa kushambulia kambi za Marekani zilizoko katika eneo la Ghuba lenye utajiri wa mafuta na kuufunga kabisa Mlango-Bahari wa Hormuz

Waziri wa Fedha wa Ufaransa Roland Lescure hata hivyo amesema leo kwamba bado hakujafikiwa uamuzi wowote "katika hatua hii" lakini mkutano wa viongozi wa G7 "bila shaka utajadili suala hili la akiba ya kimkakati". Akaongeza kuwa wanataka kutuma ujumbe wa wazi kabisa, kwamba ikiwa hawataweza kuufungua tena Mlango-Bahari huo wa Hormuz, watasafirisha mafuta kutokea kwingineko na kuyasambaza kote ulimwenguni.

Mataifa kote ulimwenguni yameendelea kuangazia namna ya kushughulikia kupanda kwa bei ya mafuta. Bangladesh imetuma jeshi lake kulinda maghala ya mafuta huku India ikiweka udhibiti mkali zaidi wa gesi asilia na ya kupikia na maafisa wa Ufaransa wamepangwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye vituo vya mafuta ili kuhakikisha bei hazipandishwi.

Mara ya mwisho, dharura kama hii ilishuhudiwa wakati Urusi ilipoivamia kikamilifu Ukraine mnamo mwaka 2022, ambapo wanachama wa IEA walitoa mapipa milioni 182.7 kufuatia kuvurugika kwa usambazaji wa nishati.