Upinzani Syria kukutana na ujumbe wa Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Upinzani Syria kukutana na ujumbe wa Urusi

Kundi kuu la upinzani la nchini Syria linaloshiriki mazungumzo ya amani yanayoendelea mjini Geneva baadae linataraji kukutana na ujumbe wa Urusi kujadili ahadi ambazo wanasema Urusi imeshindwa kuzitekeleza

Urusi ilitaka kufufua upya diplomasia tangu jeshi lake la anga liliposaidia jeshi la Syria na wapiganaji wanaounga mkono jeshi hilo, kuwaangusha waasi mjini Aleppo mnamo mwezi Disemba mwaka jana, na kuchukuliwa kama ushindi mkubwa kabisa kwa rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad kwenye mzozo uliodumu kwa miaka sita.

Pamoja na hatua hiyo ya kusimamisha mapigano, mashambulizi ya mabomu mwishoni mwa wiki iliyopita pamoja na mashambulizi ya anga nchini humo yametia doa mazungumzo yaliyoanza wiki iliyopita mjini Geneva.

"Kamati kuu ya majadiliano inayowakilisha upinzani ya nchini Syria, HNC itakutana na ujumbe kutoka wizara ya masuala ya kigeni ya Urusi, msuluhishi Mohammed Alloush ameliambia shirika la habari la Reuters.

Schweiz Syriengespräche in Genf (picture alliance/AP Photo/P. Albouy)

De Mistura anazitaka pande zote kufikia makubaliano ya kurejesha amani Syria

Baadhi ya wanadiplomasia na vyanzo kutoka upinzani wanasema HNC wanaweza kukutana na Naibu waziri wa masuala ya kigeni wa Urusi, Gennady Gatilov na mkurugenzi wa masuala ya Mashariki ya Kati wa wizara hiyo Sergei Vershinin katika siku zijazo, ingawa duru nyingine zinasema mkutano huo umepangwa kufanyika Jumatano.

Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, taarifa nyingine zinaeleza kwamba naibu kiongozi mkuu wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda Abu al-Khayr al-Masri ameuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Syria. Kulingana na mkuu wa shirika la waangalizi nchini Syria, kiongozi huyo alikuwa ni msaidizi wa kiongozi wa kundi hilo, Ayman al-Zawhiri.

Aidha, mashambulizi ya anga yaliyofanywa na vikosi vya serikali, katika eneo hilo la Kaskazini Mashariki mwa Syria yamesababisha vifo vya kiasi ya watu 11, na wengi wao wakiwa ni raia, shirika hilo limesema. wakati huohuo, jeshi limesema vikosi vyake vinazidi kuingia katika jimbo la Aleppo. 

Katika hatua nyingine, jeshi la maji la Urusi, leo hii limetuma manowari kutoka bandari ya Sevastopol iliyopo katika rasi ya Crimea na kuelekea Bahari ya Mediterrania ambako itaungana na vikosi vya wanamaji vilivyoko karibu na Pwani ya Syria.

Shirika la habari la Urusi, Interfax limemnukuu kapteni wa jeshi la maji ambaye ni msemaji wa kikosi kilichopo katika Bahari Nyeusi kwamba. manowari hiyo itakuwa ni sehemu ya vikosi vya kudumu vya maji vya nchini Urusi katika Bahari ya Mediterrania.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/APE/dpa.
Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com