1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yadaiwa kuanzisha utawala wa kabila moja

12 Septemba 2025

Upinzani Sudan Kusini umeishutumu serikali kujaribu kutekeleza utawala wa kiimla na wa kabila moja, baada ya makamu wa rais Riek Machar kushitakiwa kwa kupanga mashambulizi ya wanamgambo

https://p.dw.com/p/50OOG
Sudan Kusini Juba 2023 | Riek Machar
Kiongozi wa chama cha upinzani Sudan Kusini SPLM-IO Riek MacharPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Mashitaka dhidi ya Machar yalimfanya kiongozi huyo kuondolewa katika wadhifa wake.

Chama cha Machar cha SPLM-IO kilikanusha madai hayo pamoja na ya wanachama wengine 20. Madai yenyewe ni pamoja na mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binaadamu. Chama hicho kimesema mashitaka hayo yamebuniwa na yamenuiwa kusambaratisha makubaliano ya amani.

Hatua ya Machar kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani tangu mwezi Machi kimezua hofu ya kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kama vile vilivyoshuhudiwa mwaka 2013 hadi 2018.

Vita hivyo vilisababishwa na mvutano kati ya makabila mawili yaliyotiifu kwa viongozi hao wawili, kabila la Nuer kutoka kwa Machar na Dinka kutoka kwa hasimu wake wa muda mrefu rais Salva Kiir.