1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yajiandaa kuanza kuondoa walinda amani DR Kongo

Iddi Ssessanga
19 Desemba 2023

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa Jumanne kukubaliana na matakwa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, na kuanzisha kuwaondoa kwa taratibu askari wa kulinda amani, kuanzia baadaye mwezi huu.

https://p.dw.com/p/4aKfB
DR Kongo MONUSCO
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kuridhia uondoaji wa hatua kwa hatua wa askari wa MONUSCO nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Picha: MONUSCO/Xinhua/picture alliance

Ikiwa inakabiliwa na mzozo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, taifa kubwa na maskini itafanya uchaguzi wenye hatari kubwa wa rais na wabunge siku ya Jumatano, kura ambayo itakwenda sambamba na kumalizika kwa muda wa majukumu ya kila mwaka ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kama Monusco.

Licha ya hali tete ya ndani, serikali ya Kongo kwa miezi kadhaa imekuwa ikitoa wito wa "kuharakishwa" kujiondoa kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, kuanzia mwishoni mwa 2023 badala ya mwisho wa 2024. Inalichukulia jeshi la Umoja wa Mataifa kuwa lisilo na ufanisi katika kulinda raia dhidi ya makundi ya silaha na wanamgambo ambao wametapakaa eneo la mashariki mwa DRC kwa miongo mitatu.

Soma pia: Tshisekedi aitaka MONUSCO kuondoka haraka Kongo

Shutuma hizo ni sawa na zile zilizotolewa na nchi nyingine za Kiafrika, hasa Mali, ambayo imetaka kuondoka mara moja kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Minusma.

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi
Rais wa DR Kongo Felix Tshisekedi ameshinikiza kuondolewa kwa ujumbe wa MONUSCO, akiushtumu kutofanya vya kutosha kuwalinda raia wa Kongo dhidi ya machafuko ya makundi ya wapiganaji na waasi.Picha: Pool Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance

Katika miezi ya hivi karibuni, wanachama kadhaa wa Baraza, hasa Marekani, wameonyesha shaka iwapo vikosi vya Kongo viko tayari kuchukua nafasi ya Monusco ili kuhakikisha usalama wa watu.

Hata hivyo, kwa kuwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa hauwezi kufanya kazi bila idhini ya nchi mwenyeji, DRC inataka kulazimisha mkono wa Baraza la Usalama - ingawa ujumbe wake umekuwa mdogo kuliko wa Mali.

Hofu ya kuongezeka ghasia mashariki mwa Kongo

Hata wakati likitekeleza matakwa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Baraza hilo linatarajiwa kusisitiza "wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa ghasia" upande wa mashariki na "mvutano kati ya Rwanda na DRC," kulingana na rasimu ya maandishi ambayo shieika la AFP liliata nakala yake.

Iwapo rasimu ya azimio hilo itapitishwa kama ilivyotarajiwa Jumanne, Baraza litaamua "kuanzisha uondoaji wa taratibu, uwajibikaji na endelevu" wa ujumbe huo, kulingana na mpango wa uondoaji uliokubaliwa mnamo Novemba kati ya Kinshasa na Monusco.

Awamu ya kwanzaitahusisha kuondolewa kwa walinda amani kutoka jimbo la Kivu Kusini kufikia mwisho wa Aprili 2024, kuanzia "kabla ya mwisho wa 2023."

Soma pia: Tahadhari yatolewa dhidi ya MONUSCO kuondoka haraka Kongo

Kuanzia Mei 2024, Monusco itakuwepo Kivu Kaskazini na Ituri pekee. Na kuanzia Julai 1, nguvu yake itapunguzwa kwa takribani askari 2,350 (kutoka kiwango cha juu kilichoidhinishwa cha wanajeshi na polisi 13,800).

Uondoaji zaidi utaamuliwa kwa msingi wa ripoti ya tathmini ya awamu ya kwanza, ambayo Baraza linatarajia kuipata mwisho wa Juni 2024.

USA New York | Mkuu wa MONUSCO, Bintou Keita.
Mkuu wa MONUSCO Bintou Keita ameliambia Baraza la Usalama la UM kwamba ana wasiwasi juu ya hali ya usalama kuzorota zaidi baada ya kuondoka kwa MONUSCO DRC.Picha: Bianca Otero/ZUMA Wire/IMAGO

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kimekuwepo nchini humo tangu mwaka 1999. Kwa miaka kadhaa, Baraza la Usalama limekuwa likijitenga kwa tahadhari, likiweka vigezo vipana vya uhamishaji wa majukumu kwa vikosi vya Kongo, kwa lengo la kuanza kuondoka ifikapo mwaka 2024.

Soma pia: Maoni ya raia wa Congo baada ya kuongezwa muhula wa Monusco

Wakati mkuu wa Monusco, Bintou Keita, hivi karibuni alionyesha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa hatari ya "makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi" kati ya DRC na Rwanda, rasimu ya azimio pia inatoa wito wa "utulivu na mazungumzo" kati ya majirani hao wawili.

Bila kumtaja mtu yeyote, pia inalaani "uungwaji mkono wa chama chochote cha nje" kwa vikundi vyenye silaha vya M23 (Vuguvugu la Machi 23) na FDLR (Vikosi vya Demokrasia kwa ajili ya Ukombozi wa Rwanda), na kutoa wito wa kujiondoa kwa makundi ya kigeni kutoka eneo la Kongo.

Katika ripoti yao ya mwisho, iliyochapishwa mwezi Juni, wataalam waliopewa mamlaka na Baraza la Usalama walidai kuwa na "ushahidi mpya wa uingiliaji wa moja kwa moja kwa vikosi vya ulinzi vya Rwanda" nchini DRC, hasa katika kuyaunga mkono makundi ya M23 na FDLR.

Moto wawashwa ofisi za Monusco DRC