1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watu milioni 16 kukabiliwa na njaa Yemen

23 Septemba 2021

Mkuu wa Shirika la Chakula Duniani, WFP, ametahadharisha kwamba watu milioni 16 nchini Yemen wanaelekea kukabiliwa na ukosefu wa chakula.

https://p.dw.com/p/40iEk
Jemen Sanaa | Unterernährung
Picha: Mohammed Hamoud/AA/picture alliance

Mkuu huyo David Beasley ameongeza  kuwa, mgao wa chakula kwa mamilioni ya watu katika nchi hiyo inayokabiliwa na vita utasitishwa mwezi ujao wa Oktoba, iwapo shirika hilo halitopata fedha zaidi.

Katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusiana na mzozo wa kiutu wa Yemen, Beasley, amesema Marekani, Ujerumani, Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia pamoja na wafadhili wengine walijitokeza na kulisaidia shirika hilo lilipokuwa linakabiliwa na uhaba wa fedha mwanzoni mwa mwaka huu na janga la ukosefu wa chakula likadhibitiwa Yemen.

Umoja wa Mataifa ulitoa wito wa dola bilioni 3.85 kwa ajili ya Yemen

Kulingana namkuu huyo wa WFP, shirika hilo sasa linakabiliwa tena na uhaba wa fedha na bila ufadhili, mgao wa chakula utapunguzwa kwa watu milioni 3.2 mnamo mwezi ujao na ifikiapo Disemba, watu milioni 5 watapunguziwa chakula.

UN-Generalsekretär António Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: AFP/UN/M. Garten

Mnamo Machi Mosi, Umoja wa Mataifa ulitoa wito wa ufadhili wa dola bilioni 3.85 kwa ajili ya Yemen ila kufikia sasa zaidi ya nusu ya fedha hizo ndizo zilizochangishwa. Kulingana na Umoja wa Ulaya ulioandaa mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa hapo jana kwa ushirikiano wa Uswisi na Sweden, kiasi cha dola milioni 600 ndicho kilichochangishwa. Hii inamaanisha bado kunahitajika karibu dola bilioni moja ili kutimiza lengo la Umoja wa Mataifa. 

Marekani kupitia waziri wake wa mambo ya nje imeahidi kutoa dola milioni 290 zaidi kama msaada wa kiutu kwa Yemen na Umoja wa Ulaya nao umesema unatenga dola milioni 139 kwa ajili ya nchi hiyo.

Yemen iko kwenye mapigano tangu mwaka 2014

Mkurugenzi wa shirika la kutoa misaada ya kiutu la Oxfam nchini Yemen Muhsin Siddiquey amezitaka nchi zengine duniani kuiga mfano wa Marekani na Umoja wa Ulaya ili kuinusuru Yemen kutotumbukia katika uhaba wa chakula, umaskini na mustakabali usiokuwa na mwelekeo.

Muungano wa Saudia wakataa kusitisha mapigano Yemen

Yemen imezongwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2014 pale waasi wa Houthi wanaoungw amkono na Iran walipochukua udhibiti wa Mji Mkuu Sanaa na sehemu kubwa ya kaskazini mwa nchi hiyo na kuilazimisha serikali ya Rais Abed Rabbo Mansour Hadi kukimbilia kusini na hatimaye kuishia Saudi Arabia.

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliingia kati vita hivyo na mashambulizi ya angani ambayo yamekuwa yakifanywa na muungano huo hayajasaidia kwa njia yoyote ile, badala yake, vita vilishamiri na kusababisha mzozo mkubwa zaidi wa kibinadamu duniani.

Vyanzo: AP/AFP