1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Venezuela iliwaua raia kinyume cha sheria

Lilian Mtono
5 Julai 2019

Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaka Venezuela kusitisha mauaji ya kile ilichokielezea kama ukiukwaji mkubwa wa haki za kisiasa, kiraia na kiuchumi.

https://p.dw.com/p/3Lccp
Deutschland Berlin - Lateinamerika Karibik Initiative im Auswärtigen Amt
Picha: DW/E. Usi

Kulingana na ripoti hiyo watu hao waliuawa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita. Kamishna wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema kwenye ripoti yake mpya kwamba serikali ya Venezuela ilisajili karibu vifo vya raia 6,856, waliouawa katika kile walichodai ni makabiliano na vikosi vya usalama tangu mwanzoni mwa mwaka 2018.

Bachelet amesema akiwa mjini Geneva kwamba mauaji hayo ambayo hayakufuata sheria yaliyofanywa na vikosi vya usalama, ni kiwango cha kushtusha mno. Mwaka jana, serikali ilisajili vifo 5,287 vilivyotokea kwenye operesheni kama hizo, kati ya Januari 1 na Mei 19 mwaka huu, lakini pia vifo vingine 1,569.

Msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binaadamu, Ravina Shamdasani ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, serikali ya Venezuela iliwasilisha takwimu hizo kwa Umoja wa Mataifa baada ya kuombwa kufanya hivyo na timu ya kiufundi ya Umoja huo iliyofanya ziara nchini humo mwezi Machi. Kulingana na Shamdasani, hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza na serikali hiyo kuchapisha taarifa hizo.

Mwanasheria Karen Claderin, akiwa Caracas alisema baada ya baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo kwamba "Ninatumai kutokana na ripoti yake hiyo tutapata matokeo mazuri na muhimu. Matokeo ambayo yatatoa suluhu ama namna ambayo kimsingi itatuongoza kupata muafaka wa matatizo tunayokabiliana nayo."

Venezuela Krise Polizei
Bachelet ametaka kuachwa mara moja kwa hatua za kijeshi dhidi ya raia ili kuondoa mauaji hayo ya kiholelaPicha: picture-alliance/Zumapress/J. Wyss

Bachelet aliyezuru Venezuela mwezi uliopita, ameonya kwenye ripoti hiyo kwamba kulikuwa na sababu za kimsingi kabisa na za kuaminika kwamba mauaji hayo yalifanywa na vikosi vya usalama kinyume cha sheria.

Kulingana na ripoti hiyo, takriban watu 800 bado wako kizuizini baada ya kukamatwa kiholela, na kuongeza kuwa serikali ya rais Nicolas Maduro imeshindwa kuwahakikishia wananchi wake haki ya kupata chakula na huduma za afya. Imeripoti kuhusu kiwango cha juu cha utapiamlo na vifo vya watu 1,557 kati ya Novemba 2018 na Februari 2019, kutokana na upungufu wa vifaa tiba.

Bachelet amewataka wale wote walio na mamlaka na ushawishi ndani ya Venezuela na kwingineko kushirikiana na kuhakikisha kunapatika suluhu ya mzozo unaosababisha madhila hayo.

Wizara ya mambo ya nje ya Venezuela imewasilisha mapingamizi 70 dhidiya ripoti hiyo, na kuituhumu kwa ubaguzi na kuwa na maoni ya juujuu kuhusiana na hali halisi ya haki za binaadamu nchini humo. Kulingana na shirika la habari la AVN, taarifa ya wizara hiyo imesema ripoti hiyo imeonyesha kuvipendelea vyanzo vyake na imekosa uhalisia.