1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vimeufanya mzozo wa Venezuela kuwa mkali

Josephat Charo
6 Machi 2019

Mkuu wa Shirika la kutetea haki la Umoja wa mataifa Michelle Bachelet alisema siku ya Jumatano kwamba vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Venezuela vimechochea kuukuza mgogoro unaoikabili nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/3EYLr
Burundi l Menschenrechtsbüro der UNO geschlossen l Michelle Bachelet
Picha: Reuters/D. Balibouse

Katika ripoti yake ya mwaka kwa baraza la Umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamu Mkuu wa baraza hilo pia amemkosoa vikali rais Maduro. Bachelet amesema ni wazi kwamba Venezuela inaonesha ni kiasi gani uvunjwaji wa haki za binadamu na haki za kisiasa, ikiwa ni pamoja na kuwanyima watu uhuru, vinaweza kusababisha anguko la kiuchumi na haki za jamii.

Wananchi wa Venezuela, wanaokabiliwa na mdororo wa uchumi na mtikisiko wa kisiasa wanapambana kupata mahitaji muhimu yakiwemo chakula na dawa.

Serikali ya Marekani ambayo inamuunga mkono kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo, Juan Guaido, kuwa ndiye kiongozi wa nchi hiyo, iliweka vikwazo kwa kampuni ya mafuta ya serikali ya Venezuela, PDVSA, mwezi Februari. Marekani pia imempatia Juan Guaido mamlaka ya kuzitumia akaunti za serikali ya Venezuela zilizo nchini humo.

Kiongozi huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 35 anayetambuliwa na zaidi ya nchi 50 kuwa ndiye kiongozi halali wa nchi hiyo, alikiuka marufuku ya serikali ya kutokusafiri na kuongoza maandamano yaliyounga mkono jitihada zake za kumuondoa madarakani Maduro. Juan Guaido aliondoka nchini mwake na kufanya ziara ya siku kumi kutembelea nchi za Amerika ya kusini zinazomuunga mkono. 

Venezuela PK von Juan Guaido in Caracas
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Juan Guaido (katikati)Picha: imago/R. Pena

Kwa upande wake rais Maduro amewataka raia wanaomuunga mkono kufanya maandamano ya kumpinga Guaido Jumamosi ili kuyazima maandamano ya kiongozi huyo wa upinzani na kuadhimisha miaka minne tangu rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, alipotangaza kuiwekea vikwazo serikali ya Venezuela.

Mwakilishi wa Marekani katika mgogoro wa Venezuela, Elliot Abrams, alisema siku ya Jumanne kuwa serikali yake inafikiria kutoa adhabu zaidi kwa Venezuela ili kuongeza shinikizo kwa Maduro.

Marekani bado haijaondoa wazo la kuweka vikwazo vingine ambavyo huenda vikayalenga makampuni ya kigeni ama mataifa mengine yenye ushirikiano wa kibiashara na Venezuela inayokabiliwa na umasikini kutokana na mgogoro unaoendelea. Zaidi ya raia milioni 2.7  wanakadiriwa kuikimbia nchi hiyo tangu mwaka 2015.

(afpe)