1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waandaa mikutano zaidi kuhusu wahamiaji

Admin.WagnerD22 Septemba 2015

Umoja wa Ulaya unafanya mikutano miwili ya dharura wiki hii kwa lengo la kutatua tafauti zao juu ya mzozo mbaya kabisa wa wakimbizi kulikabili bara hili tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia,

https://p.dw.com/p/1GaNT
Wahamiaji wakidandia treni Croatia kuelekea Hungary.
Wahamiaji wakidandia treni Croatia kuelekea Hungary.Picha: Getty Images/J. J. Mitchell

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akizungumizia mikutano hiyo hapo Jumatatu amesema "Mashauriano haya yatakuwa muhimu lakini hayatopelekea kulitatua tatizo tunalokabiliana nalo.Haiwezekani na hakutakuwepo kwa ufumbuzi utakaopatikana kwa kucha moja.Mikutano na majadiliano zaidi itafuatia.Tutahitaji subra."

Mikutano hiyo ambayo inaitishwa wakati nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya wakilaumiana kwa kushindwa kukabiliana na mzozo huo unaoepelekea wahamiaji hao kuvamia uzio wenye senyen'ge katika juhudi za kuingia Ulaya,kupoteza maisha kwa kukosa pumzi wakiwa wamejazana kwenye malori na maiti zao zikikutwa zikielea fukweni mwa bahari.

Bila ya shaka kutochukuliwa kwa hatua ya kukabiliana na hali hiyo hakutokomesha wimbi hilo la wahamiaji na wakimbizi wanaokimbilia Ulaya na wala hakutozifariji serikali za nchi wanachama wa umoja huo zenye kujaribu kulipunguza wimbi hilo.

Zaidi ya watu 6.000 wanaweza kuwasili nchini Ugiriki Jumanne pekee wakati mawaziri wa mambo ya ndani watakapokutana mjini Brussels Ubelgiji na Jumatano wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya watakapokuwa na mkutano wao wa kilele kujadili mipango ya sera za kipindi cha kati na muda mrefu.

Kutopewa uzito unaostahiki

Mshauri wa Shirika la Madaktari wasiokuwa na Mipaka Aurelie Ponthieu akizungumza baada ya kukitaarifu kikao cha bunge la Ulaya wiki iliopita kuhusu juhudi za uokozi bahari ya Mediterenia kikao ambacho kilikuwa kitupu kwamba majadiliano hayo yako mbali kabisa na uhalisia.Badala ya kuhudhuria kikao hicho takriban wabunge wengi wa Ulaya na maafisa waandamizi waliamua kwenda kujipatia chakula cha mchana.

Polisi ikijaribu kudhibiti wahamiaji Croatia.
Polisi ikijaribu kudhibiti wahamiaji Croatia.Picha: Getty Images/J. J. Mitchell

Mashirika ya misaada yamekuwa yakiusihi Umoja wa Ulaya kuwatengea njia salama wahamiaji hao wanaokimbilia Ulaya wakati shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa linautaka umoja huo kuwachukuwa wakimbizi wa Syria walioko katika nchi za Mashariki ya Kati na Uturuki.

Wakati ikikabiliwa na hali hiyo ya dharura ya kibinaadamu Umoja wa Ulaya badala ya kuchukuwa hatua kukabiliana na changamoto hiyo kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa miongo mingi barani Ulaya umoja huo umekuwa ukiipa kipau mbele mijadala kuhusu sera na umoja.

Sera ya pamoja

Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk katika taarifa yake ya mwaliko kwa viongozi kwa mkutano wa kilele wa kesho amesema ni muhimu kuanzisha sera ya uhamiaji ya kuaminika na kwamba tafauti miongoni mwao kuhusu wahamiaji haziwezi kuwa kisingizio cha kutokuwa na mkakati kabambe wa pamoja au kutengeneza sera madhubuti ambayo itakuwa na ufanisi,inawajibika na wakati huo huo kuheshimu maadili yao ya msingi.

Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk.
Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk.Picha: picture alliance/augenklick/S. Minkoff

Nchi za Umoja wa Ulaya zinatafautiana sana linapokuja suala la kuwajibika kwa pamoja kuwapokea maelfu ya wahamiaji wanaokuja Ulaya ambapo theluthi mbili kati yao wanastahiki kupatiwa hifadhi au aina fulani ya ulinzi wa kimataifa.

Jamhuri ya Czech,Hungary na Slovakia zinapinga kabisa mpango wa lazima wa mgao wa wahamiaji baina ya nchi wanachama wakati Poland, Latvia na Estonia pia zina mashaka na mpango huo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP

Mhariri: Mohammed Khelef