Ulaya yampa heshima za mwisho Helmut Kohl | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ulaya yampa heshima za mwisho Helmut Kohl

Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl atakuwa kiongozi wa kwanza kuandaliwa mazishi rasmi ya Umoja wa Ulaya, kufuatia mchango alioutoa katika kuliunganisha bara hilo baada ya vita vikuu vya pili.

Deutschland | Portrait von Helmut Kohl im Kanzleramt (picture-alliance/NurPhoto)

Helmut Kohl anasifiwa kwa mafanikio kisiasa, nchini Ujerumani na barani Ulaya kwa Ujumla

Viongozi wengi wa Ulaya, wakiwemo wa sasa na wa zamani, wamekusanyika katika jengo la Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, Ufaransa, kumpa Kohl heshima zao za mwisho. Kohl aliaga dunia tarehe 16 Juni, 2017 akiwa na umri wa miaka 87.

Kutoka Strasbourg, mwili wake utasafirishwa kurudi nyumbani Ujerumani, na atazikwa katika makaburi ya Kanisa Kuu la Kikatoliki katika mji mkongwe wa Speyer. Lakini kiongozi huyo hatakumbukwa tu kwa mafanikio yake kisiasa, na heshima kubwa aliyopewa wakati wa mazishi.

Kuanzia orodha ya wazungumzaji kwenye msiba kupitia mahala unapofanyika msiba huo na pia migogoro ya muda mrefu ndani ya familia, kifo cha Helmut Kohl kinaonekana kutonesha madonda zaidi kuliko kutoa heshima kwa mchango wa mwanasiasa huyo.

Katika kutoa heshima za mwisho kwa hayati Helmut Kohl umezuka mzozo mkali wa kisiasa na kifamilia. Kansela wa sasa Angela Merkel, ambaye Kohl alikuwa akimtaja kama binti yake, hatakiwi kuhutubia katika msiba huo, kwa mujibu wa jarida la habari la Der Spiegel.

Uhusiano mgumu kati ya Kohl na Merkel

Trauer nach dem Tod von Helmut Kohl - Kondolenzbuch - Merkel und Steinmeier (picture-alliance/dpa/S. Kembowski)

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akisaini katika kitabu cha kumbukumbu baada ya kifo cha Helmut Kohl, akitazamwa na Kansela Angela Merkel

Uhusiano kati ya Merkel na kansela huyo wa zamani ulipungua  kwa kiasi kikubwa baada ya Kohl kustafu siasa mwaka 2002. Katika kadhia ya ufadhili wa chama cha CDU mwishoni mwa utawala wake, Merkel alimlaumu Kohl kwa kukisababishia madhara chama hicho cha kihafidhina. Na muda mfupi baadaye Merkel alichukuwa uwenyekiti wa chama hicho na hatimaye kuwa kansela wa kwanza mwanamke wa Ujerumani.

Ingawa alimtembelea katika siku yake ya kuadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa mwaka 2010 na kumshukuru hadharani kwa mchango wake katika kunusuru maisha ya mamilioni ya raia walioishi Ujerumani Mashariki hadi mwaka 1990, akiwemo kansela Merkel mwenyewe, Kohl hakuwahi kumsamehe Merkel, na kwa mujibu wa mjane wake Maike Kohl-Richter, alikataa katakata ,  pendekezo la Merkel kuwa mmoja wa wazungumzaji kwenye msiba wake.

Bibi Kohl-Richter alikanusha kuwepo mgogoro kati yake na Merkel kuhusu msiba wa Helmut, lakini alibainisha kuwa katika kuamua mwili wake uagwe Strasbourg, mume wake alitaka kuadhimisha mchango wake wa kihistoria kwa Umoja wa Ulaya, uliojengwa kwa ushirikiano wa karibu na Ufaransa na rais wake Francoise Mitterrand. Lakini ripoti zikazagaa haraka kwamba Kohl - mtu aliefahamika sana kwa kuweka visasi - alikuwa pia analipa kisasi dhidi ya wanasiasa mjini Berlin, akiwemo Merkel na rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier.

Tangu alipopata ajali miaka michache iliopita, Kohl alikuwa akitumia baiskeli ya walemavu na mke wake hakumuruhusu kuzungumza hadharani, na alichukuwa jukumu la kusimamia maslahi yake yote.

Viongozi muhimu kumuaga Kohl

Kaiser-Dom zu Speyer (picture-alliance/dpa/U. Anspach)

Helmut Kohl atazikwa katika makaburi ya Kanisa Katoliki la mjini Speyer

Katika wadhifa wake kama kansela wa Ujerumani Merkel atazungumza katika shughuli za mjini Strasbourg, ambako pia watazungumza rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, raia wa Ufaransa Emmanuel Macron na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton.

Siku ya Jumanne, wabunge wa Ujerumani walishiriki katika hafla ya kumuaga Kohl iliofanyika katika majengo ya bunge - Bundestag mjini Berlin, ambayo ilikuwa kama kivuli cha tukio kuu la Umoja wa Ulaya mjini Strasbourg. Akigusia juu ya mgogoro huo, Spika wa bunge la Ujerumani Nobert Lamert alisifu mchango wa kansela huyo wa zamani, lakini akasema: Njia ya Kohl iliijaa majeraha - yale yaliompata mwenyewe, na ambayo aliwasababishia wengine.

Akizungunzia msiba uliogubikwa na mivutano, Lamert aliashiria kwamba Berlin ndiyo ilipaswa kuwa na jukumu kubwa zaidi - akisema mahala na namna ya kumkumbuka mchangiaji mkubwa kwa Ujerumani halikuwa suala tu la kifamilia. Alionekana pia kumuunga mkono rais Steinmeier, aliekaa karibu naye, kwa kusema kuwa Bundestag ndiyo pangekuwa mahala bora zaidi kwa tukio kama hilo, "akiwepo rais wa shirikisho."

Siyo katika siasa pekee ambako kifo cha Kohl kimedhihirisha mgawanyiko wa wazi. Kimeonyesha pia mgogoro wa muda mrefu ndani ya familia yake, ikiwemo kati ya bibi Kohl-Richter na Walter na Peter, watoto wake wawili kutoka ndoa yake ya kwanza iliohitimishwa na kifo cha mke wake wa kwanza Hannelore mwaka 2001.

Wiki iliopita Walter Kohl na wanae walikwenda nyumbani kwa bibi Richter-Kohl na hayati Helmut Kohl walikokuwa wakiishi pamoja ili kutoa heshima zao za mwisho lakini walizuiwa katika tukio lililorekodiwa na vyombo vya habari vya Ujerumani.

Mwandishi:Maximilian Koschyk/Sertan Sanderson

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Saumu Yusuf

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com