1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yajaribu kuwasajili wapiganaji wa kiafrika

9 Machi 2022

Nigeria, Senegal na Algeria zimekosoa juhudi za Ukraine za kusajili wapiganaji wa kiafrika dhidi ya uvamizi wa Urusi. Wachambuzi wa mambo wanasema walioitikia wito huo wanahitaji kufikiria upya.

https://p.dw.com/p/48Cp5
Luhansk I Mobilisierte Soldaten
Picha: Stanislav Krasilnikov/ITAR-TASS/imago images

Vita ya Urusi nchini Ukraine imeingia wiki ya pili lakini Kyiv tayari inawavutia wapiganaji wa kigeni kutoka mataifa ya afrika, ambapo baadhi ya vijana wanazingatia kujiunga katika mapambano hayo endapo kutatokea fursa. 

"Kama Ukraine itaamua kunilipa pesa nzuri, ambayo najua siwezi kuipata hapa, kiukweli nitaenda na kupigana". Huyo ni Kimanzi Nashon mwanafunzi katika jiji la Nairobi Kenya akielezea utayari wake wa kujiunga na Ukraine katika vita inayoendelea. Anaongeza kuwa

"Tunatumai kwamba tutalipwa kabla ya kwenda huko, na kisha vita iiishe kabla ya kutokea chochote, nitakuwa mwenye furaha na nitarudi Kenya nikiwa milionea"

Si Nashon pekee mwenye fikra kama hizo za kujiunga na vikosi vya Ukraine. Beatrice Kaluki ambaye hana ajira aliieleza DW kwamba ikiwa fursa kama hiyo itajitokeza ya kwenda Ukraine kama mamluki, basi ataikimbilia.Maoni: Mshikano una kasoro unapowaacha nyuma Waafrika Ukraine

"Bora nife katika uwanja wa mapambano huko Ukraine nikijua kwamba familia yangu itapewa fidia hata baada ya mimi kufa, kuliko kufa hapa Kenya kwa msongo wa mawazo kwasababu ya kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira".

Vijana hawa walikuwa wakiitikia wito wa rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alioutoa wiki iliyopita wa kuwaita watu kujiunga na nchi yake katika kupambana na uvamizi wa Urusi. Kulingana na Ryan Cummings, ambaye ni mkurugenzi wa shirika la ushauri na usimamizi wa usalama Signal Risk, lenye makao yake makuu Afrika Kusini, rais Zelenskyy anaweza kutumia changamoto za hali ya kijamii na kiuchumi barani Afrika kuwarubuni wapiganaji wa kiafrika kwenda Ukraine.

Prorussische Truppen im Gebiet Donezk stationiert
Vikosi vyenye kuunga mkono Urusi huko DonezkPicha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Mafao yanaweza kutokana na wao kupewa uraia wa Ukraine au kupewa aina fulani ya fidia ya kifedha kwa kushiriki katika mzozo kwa niaba ya vikosi vya Ukraine. Mtaalamu huyo wa usalama anasema nchi za kiafrika zinapaswa kuzingatia athari za kuruhusu raia wake kujiunga na vita hiyo.

"Ni dhahiri Urusi imesema kwamba mtu yeyote au nchi itakayoisaidia Ukraine katika vita hii au operesheni ya kijeshi ambayo Kremlin imeianzisha dhidi ya Ukraine, itachukuliwa kuwa iko vitani na Urusi."

Hata hivyo nchi za kiafrika zimepinga vikali wito wa Ukraine wa kuwavutia wapiganaji wa kiafrika kujiunga na "jeshi la kimataifa" dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Siku ya Jumatatu, Nigeria ilitoa onyo kali kupitia ukurasa wa Twitter kwa raia wake kwamba haitovumilia usajili wowote wa mamluki kwenda kupigana kando ya vikosi vya Ukraine dhidi ya vile vya Urusi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Nigeria Francisca Omayuli amesema kuwa nchi yake haitoruhusu raia wake kujitolea kama mamluki. Kulingana na gazeti la kila siku la Nigeria la The Guardian, wiki iliyopita zaidi ya vijana 100 walijiandikisha na kuonyesha nia ya kwenda kupigana Ukraine katika ubalozi wa mjini Abuja.

Serikali za Afrika zaanza kuhangaika kuondoa raia wao UkraineSenegal nayo imeelezea kutoridhishwa kwake na serikali ya Ukraine, ikisema kwamba vijana wapatao 36 hivi wameonyesha nia ya kupambana na majeshi ya Urusi. DW ilijaribu kuwatafuta vijana hao lakini bila ya mafanikio. Wizara ya Mambo ya nje ya Senegal ilisema kuwa ilishangazwa kujua kwamba Ubalozi wa Ukraine mjini Dakar ulichapisha ombi kwenye ukurasa wake wa Facebook kwa raia wa kigeni kujiunga na  jeshi la Ukraine.

Katika taarifa yake, serikali ya Senegal ilikosoa mpango huo na kuwaonya raia wake kwamba kuajiri watu wa kujitolea, mamluki au wapiganaji wa kigeni katika ardhi ya Senegal ni kinyume cha sheria. Ingawa Ubalozi wa Ukraine mjini Dakar umefuta tangazo hilo la Facebook, lakini utayari wa baadhi ya vijana wa kiafrika kujiunga na vita hiyo unaibua maswali mengi.

Senegal, ambayo ina uhusiano mkubwa wa kisiasa na kijeshi na Urusi, ilikuwa moja ya nchi 17 za Kiafrika ambazo zilijizuia kupiga kura juu ya azimio la Umoja wa Mataifa la Machi 2 kulaani uchokozi wa Urusi na kutaka mapigano yasitishwe. Algeria ambayo ni mteja mwingine wa vifaa vya kijeshi vya Urusi pia ilitoa wito kwa Ukraine kuacha kujaribu kusajili wapiganaji kutoka nchi yake. Serikali yake pia imekaa kimya kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Mitandao ya kijamii nayo imegeuka uwanja wa mapambano kati ya wale wanaounga mkono Ukraine na upande mwingine Urusi.