1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatuma wanajeshi, mitambo ya Patriot Uturuki

Klaus Jansen8 Januari 2013

Jeshi la Ujerumani leo (08.01.2013) limetuma wanajeshi wa kwanza nchini Uturuki, kama sehemu ya makubaliano ya Jumuiya ya Kujimhami NATO, kuilinda nchi hiyo dhidi ya makombora kutoka Syria.

https://p.dw.com/p/17Fl6
Wanajeshi wa Ujerumani wakiiandaa mitambo ya kuzuia makombora, maarufu kama Patriot.
Wanajeshi wa Ujerumani wakiiandaa mitambo ya kuzuia makombora, maarufu kama Patriot.Picha: Deutsche Bundeswehr/Getty Images

Wanajeshi hao karibu 40 wameungana na wenzao kutoka Uholanzi, nchi nyingine inayomiliki mitambo ya Patriot, inayotumika kuzuia makombora. Mitambo ya Patriot ya Ujerumani pia inasafirishwa leo kuelekea nchini Uturuki.

Serikali yasisitiza wanajeshi wake hawaendi kupambana

Serikali ya Ujerumani imekuwa ikisisitiza mara kwa mara: kwamba kupelekwa kwa wanajeshi wake katika mpaka wa Uturuki na Syria si kwa nia ya kushiriki mapambano. Imesema wanajeshi hao hawatajihusisha na mgogoro unaoendelea nchini Syria, na hili ndio jambo ambalo waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere amelipa umuhimu katika ufafanuzi wa mpango huu. "Harakati hizi ni makhsusi kwa ulinzi na hatua za tahadhari katika eneo la NATO, na hapa kwa ajili ya kulinda mipaka ya Uturuki," amesema waziri De Maziere.

Uturuki  ikiwa ni mwanachama wa NATO  iliwaomba washirika wake kuisadia na sasa ombi hilo limejibiwa. Wanajeshi wa kwanza  wa Ujerumani wanawasili nchini humo na watafanya kazi na wanajeshi wa Uholanzi kuandaa eneo itakapowekwa mitambo hiyo ya Patriot. Mitambo ya Ujerumani inasafirishwa leo kwa njia ya bahari kutoka bandari ya Travemünde kuelekea nchini Uturuki. Awamu nyingine ya wanajeshi wa Ujerumani yenye jumla ya wanajeshi 350 watapelekwa nchini Uturki wiki ijayo.

Dhamira hii ni ishara muhimu ya mshikamano na Uturuki, amesema waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle na kuongeza kuwa: "Tusisahau kuwa kuna mauaji yamefanyika nchinin Uturuki kutokana na mashambulizi kutoka Syria. Hili ndiyo hasa linaloipa wasi wasi Uturuki, kwa sababu hakuna anayejua utawala wa Syria bado unaweza kufanya nini."

Wanajeshi wa Ujerumani wakiwa katika moja ya mitambo ya kuzuia makombora ya Patriot.
Wanajeshi wa Ujerumani wakiwa katika moja ya mitambo ya kuzuia makombora ya Patriot.Picha: Getty Images

Uwezo wa mitambo ya Patriot

Katika  kuilinda Uturuki, mitambo hiyo ya Patriot inaweza kuzuia mashambulizi ya roketi, makombora ya masafa marefu na hata kuyadungua baadhi yake. Lakini mitambo hiyo haiwezi kuzuia kitisho kikubwa kama vile mashambulizi ya mizinga. Kwa hivyo hatua hii inapaswa kueleweka kuwa ni ya kiishara zaidi, na kazi yake hasa ni kuzuia, amesema waziri wa ulinzi Thomas de Maziere.

Ujerumani itaiweka mitambo yake katika eneo la Kahramanmaras, karibu kilomita 100 kutoka mpaka wa Syria. Hii ndiyo operesheni ya kwanza ya kweli kwa mitambo ya patriot kutumika baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa. Bunge la Ujerumani lilipiga kura kwa wingi katikati ya mwezi Disemba kuruhusu kupelekwa kwa mitambo hiyo, na imeruhusiwa kukaa huko hadi mwezi Februari mwaka 2014.Gharama za operesheni hiyo kwa serikali ya Ujerumani zinakadiriwa kuwa euro milioni 25.

Mwandishi:Leone Stebe/Iddi Ssessanga
Mhariri:Yusuf Saumu