Ujerumani na Kenya zatambua dhima ya UN
21 Januari 2026
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Johann Wadephul ameanza hivi leo ziara yake ya siku mbili katika kanda ya Afrika Mashariki, akizitembelea Kenya na Ethiopia.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Ujerumani ametilia mkazo umuhimu wa dhima ya Umoja wa Mataifa katika kuitatuwa migogoro ya ulimwengu huku ukiweko wasiwasi kwamba rais wa Marekani Donald Trump huenda anapanga kuunda chombo cha kukinzana na Taasisi hiyo ya dunia.
Ujerumani yatoa wito wa mageuzi makubwa kwenye Baraza la Usalama la UN
Ametowa mtazamo huo pamoja na mwenzake wa Kenya Musalia Mudavadi walipokutana mjini Nairobi. Wadephul pia anakutana na rais William Ruto hivi leo.
Msimamo wa Ujerumani na Kenya kuhusu umuhimu wa Umoja wa Mataifa umekuja chini ya kiwingu cha wasiwasi uliosababishwa na hatua ya Trump ya kuunda bodi ya amani ambayo itawajibika kusimamia juhudi za ujenzi mpya wa eneo la Ukanda wa Gaza baada ya vita.