1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki na wakopeshaji wake washindwa kufikia makubaliano

Admin.WagnerD4 Juni 2015

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras amesema makubaliano kati ya nchi yake na wakopeshaji wake yako karibu kufikiwa baada ya kufanya mkutano na maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya jana usiku.

https://p.dw.com/p/1FbfR
Picha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Licha ya kaminsheni ya Umoja wa Ulaya kutoa tamko kusema hatua zimepigwa kati yake na Ugiriki katika kuelewa msimamo wa kila mmoja, serikali ya mrengo wa kushoto ya Ugiriki bado imekatalia mbali mapendekezo ya kubana matumizi na kuongeza kodi, masharti ambayo wakopeshaji wake Umoja wa Ulaya, benki kuu ya Umoja wa Ulaya na IMF inataka yatamizwe kabla ya kuipa nchi hiyo mkopo mwingine ili kuiepusha nchi hiyo kufilisika na kuiyumbisha kanda inayotumia sarafu ya euro na masoko ulimwenguni.

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker ambaye alimualika waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras kwa dhifa ya chakula cha jioni hapo jana katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels anatarajiwa kuitisha mkutano mwingine katika siku za hivi karibuni.

Mazungumzo yanatarajiwa kuendelea

Junker ambaye ameyataja mazungumzo kati yake na Ugiriki kuwa yaliyo na changamoto amesema bila shaka mazungumzo hayo yataendelea baada ya kutofikia makubaliano yoyote na waziri mkuu Tsipras na kuongeza kilichomfanya kuondoka kutoka mazungumzo ya jana usiku ni kwasababu alihitaji kupata usingizi baada ya kushauriana kwa muda mrefu na kiongozi huyo wa Ugiriki na alihitaji kujiandaa kwa ajili ya duru nyingine ya mazungumzo.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Huku mgogoro wa kiuchumi unaoikumba Ugiriki ukizitia nchi wanachama wa kanda ianyotumia sarafu ya euro wasiwasi pamoja na Umoja wa Ulaya na Marekani, Chama tawala nchini Ugiriki cha Syriza kinajaribu kudumisha uungwaji mkono wa wapiga kura waliokichagua kuingia madarakani mwezi Januari mwaka huu kwa msingi wa ahadi ya kukomesha mpango wa kubana matumizi.

Msemaji wa chama hicho bungeni Nikos Filis ameliambia shirika la habari nchini humo kuwa serikali haitakubali kutia saini makubaliano yoyote yanayoibana na itakuwa bora kuandaa chaguzi mpya nchini humo iwapo watahisi kufinyiliwa katika kona.

Naibu wa waziri anyesimamia shughuli za meli Ugiriki Thodoris Dritas amesema nchi yake haitakubali masharti yanayotolewa na Junker ya kufanya mageuzi magumu ili nchi hiyo ipate mikopo zaidi na kusisitiza Ugiriki haitasalimu amri kwa kukubali masharti ya wakoposhaji wake wa kimataifa yanayopendekezwa katika mazungumzo.

Ugiriki ina imani itasaidika

Hata hivyo Tsipras amesema wiki hii wakopeshaji wake wamekuwa wakiandika mapendekezo yao na serikali ya Ugiriki pia ikifanya hivyo juu ya masuala yanayoleta utata na anatumai kuwa mapendekezo yao yatakubalika.

Tsipras na Junker katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya,Brussels
Tsipras na Junker katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya,BrusselsPicha: Reuters

Hali kadhalika Ugiriki imesema italipa sehemu ya deni lake kwa shirika la fedha duniani IMF hapo kesho

Junker amefutilia mbali hofu kuwa Ugiriki italazimika kujiondoa kutoka kanda inayotumia sarafau ya euro, suala ambalo maafisa wengi wa Umoja wa Ulaya wanahofia huenda likahujumu uthabiti wa muda mrefu wa kanda hiyo.

Vyombo vya habari nchini Ugiriki vimeripoti hii leo kuwa vinatarajia makubaliano kufikiwa ifikapo tarehe 14 mwezi huu, huku maafisa wa ngazi ya juu wa kanda inayotumia sarafu ya euro wakitarajiwa kufanya mkutano kwa njia ya simu hii leo kuujadili mzozo huo wa Ugiriki.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Iddi Ssessanga