Uganda yashinikizwa kutambua haki ya mashirika yasio ya kiserikali | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Uganda yashinikizwa kutambua haki ya mashirika yasio ya kiserikali

Shirika la kutetea haki za kibinaadamu Human Rights watch limesema mashirika ya utafiti na mashirika mengine yasio ya kiserikali yananyanyaswa vikali na serikali ya Uganda.

Nembo ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch

Nembo ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch

Ripoti ya shirika hilo iliotolewa hii leo imesema kuwa mashirika hayo hivi karibuni yamekuwa yakinyimwa haki ya kufanya mikutano nchini humo.

Mashirika yasio ya kiserikali nchini Uganda yakiwemo yale ya utafiti mara kwa mara yamekuwa yakinyimwa haki ya kufanya mikutano kwa kufungiwa mikutano hiyo, vitisho, kufungwa jela na hata kuingiliwa katika shughuli zao za kila siku.

Sasa ripoti ya shirika la kutetea haki za kibinaadamu la human rights watch ilio na kurasa 50, imesema ni lazima serikali hiyo kuwacha unyanyasaji kwa kuwa mashirika kama hayo yana haki ya kufanya chochote ikiwemo kuwa na mikutano. Shirika hilo limesema kwa serikali ya Uganda kufanya hivyo basi moja kwa moja itakuwa inaingilia uhuru wa kuzungumza au kutoa maoni.

Neela Ghoshal mtafiti katika shirika la Human Rights Watch amesema wangelipenda Museveni na maafisa wengine wa serikali kutambua mashirika yasio ya kiserikali, na pia kuwacha kutuma habari za vitisho kwa mashirika hayo. Neela amesema mashirika hayo yana haki ya kukutana hata kama wanazungumzia maswala nyeti kama ya wasagaji na mashoga au suala la ardhi.

Mashirika ambayo yanalengwa na serikali hiyo ni yale yanayojishughulisha na uwazi katika mapato yanayotokana na biashara ya mafuta, maswala ya ardhi, madadiliko katika maswala ya sheria na utawala bora na hata kulinda haki ya binaadamu haswa haki ya mashoga na wasagaji. Shirika la Human Rigths watch linasema mawaziri katika serikali hiyo pamoja na maafisa katika mikoa wamekuwa mstari wa mbele kutekeleza unyanyasaji huo.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Neela Ghoshal anasema hatua ya serikali ya Uganda inayochukua ni kwa sababu mashirika haya yanaaingilia maswala yao kisiasa na pia kifedha ambayo huwafaidisha wao wenyewe na sio kwa ajili ya wananchi wanaowaongoza.

Rais Yoweri Museveni aliyechukua madaraka nchini Uganda tangu mwaka wa 1986 anaonekana kujitayarisha kuwania tena muhula mwengine. Lakini tangu kuchaguliwa tena kwake mwaka wa 2011 kumekuwa na wasiwasi mkubwa nchini Uganda juu ya namna siasa zinavyoendeshwa huku raia nchini humu wakiishutumu vikali serikali hiyo namna inavyoendesha majukumu yake.

Idadi kubwa ya mashirika yasio ya kiserikali huendesha kazi zao nchini Uganda lakini serikali inatoa nafasi tu kwa wale wanaotoa huduma kwa raia na wale wote wanaojikita katika maswala nyeti kama ya ardhi na namna fedha za serikali zinavyotumiwa na hata mabadiliko ya kisiasa, serikali ya Yoweri Museveni kamwe haitoi fursa kwa mashirika hayo kufanya kazi kwa uhuru nchini humo.

Sasa serikali ya nchi hiyo imetakiwa kubadilisha mwenendo wake kwa mashirika yasiyo ya kiserikali na kuyapa nafasi ya kufanya kazi yao bila ya kunyanyaswa.

Mwandishi: Amina Abubakar/Human Right Watch Report

Mhariri: Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com