1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yapata spika mwingine mwanamke

Lubega Enmmanuel25 Machi 2022

Kama ilivyobashiriwa mara tu baada ya chama chake kumteua, Anita Among amechaguliwa na idadi kubwa ya wabunge kuwa spika mpya wa bunge la Uganda.

https://p.dw.com/p/493JD
Uganda I Parlamentswahlen
Picha: Parliamentary Press Office/Uganda

Hiyo ni hatua ya kuhesabu kura za wagombea kiti cha spika wa bunge. Wagombea Anita Among wa chama tawala cha NRM na Asuman Basarirwa aliyeshikilia bendera ya upinzani walichuana katika kinyang'anyiro hicho. Raia wengi wa Uganda walikuwa wamemtabiria Among kushinda kutokana na chama chake cha NRM kuwa na idadi kubwa ya kubwa ya wabunge ambao ni zaidi ya asilimia 80 katika bunge hilo.

Anita Among amepata kura 401 za ushindi huku mpizani wake Asuman Basalirwa akipata kura 66. Huyu hapa jaji mkuu akimtangaza Anita Among mshindi.

Kulingana na kura alizopata Asuman Basalirwa imedhihirika kuwa upinzani wenye idadi ya zaidi ya wabunge mia moja haujaungana wala kuwashawishi wabunge wa chama tawala kumpigia kura. Yumkini nao walifahamu kuwa ingekuwa vigumu kumshinda mgombea wa chama tawala.

Soma pia→Spika Jacob Oulanya atakumbukwa kivipi Uganda ?

Mwanamke wa pili kuchaguliwa kuwa Spika

Mjadala ndani ya Bunge la Uganda
Mjadala ndani ya Bunge la UgandaPicha: Reuters/J.Akena

Mara tu baada ya kutangazwa mshindi, Anita Among aliapishwa ili kuweza kuendesha shughuli za bunge akikabidhiwa wadhifa huo rais Museveni pamoja na jaji mkuu Owiny Dolo.  Hii ni mara ya pili kwa mwanamke kushikilia wadhifa wa spika Uganda.

Rebecca Alitwala Kadaga ndiye alikuwa wa kwanza na kushikilia wadhifa huo akiwa spika kwa muda wa miaka 10. Hata hivyo alishindwa katika jaribio lake la kutaka  kuendelea kwenye wadhifa huo wakati chama tawala NRM kilipomteua naibu wake Jacob Oulanya ambaye sasa ni marehemu.

Soma pia→Spika wa bunge la Uganda afariki dunia

Kifo cha Oulanya aidha kimeshuhudiwa kuibua mabishano ya kikabila pale jaji mkuu Owiny Dollo alipowashtumu watu aliodai ni wa jamii ya Baganda kwa kufanya maandamano Marekani wakipinga kupelekwa kwa Jacob Oulanya huko kwa matibabu.

Hadi wakati wa kuandaa taarifa hii zoezi la kumchagua naibu spika kati ya mbunge Thomas Tayebwa wa chama cha NRM na Moses Okot Bitek wa upinzani lilikuwa likiendelea.