1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda: HRW yataka uchunguzi kifo cha mwanaharakati

Sylvia Mwehozi
15 Oktoba 2019

Shirika la Human Right Watch, limetoa wito kwa serikali ya Uganda kufanya uchunguzi wa kina juu ya kifo cha mwanaharakati wa kutetea haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja kilichotokea Oktoba 4.

https://p.dw.com/p/3RIoA
Uganda Entebbe | LGBT Pride Feier
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Vassie

Kifo cha mwanaharakati Brian Wasswa kinakuja mnamo serikali ya Uganda ikipanga kuwasilisha tena muswada wa kupinga vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, muswada ambao utatoa adhabu ya kifo kwa watu watakaokutwa na hatia ya vitendo hivyo.

Waswa alishambuliwa nyumbani kwake mjini Jinja, mashariki mwa Uganda. Alikuwa mtetezi wa jamii za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja pamoja na kuwa mshauri wa watu walio na maambukizi ya HIV.

Siku kadhaa baada ya kifo chake, waziri wa maadili wa Uganda, Simon Lokodo aliwaeleza wandishi wa habari kwamba bunge linapanga kuwasilisha muswada utakaohalalisha hukumu kwa wale wanaotetea vitendo hivyo, ikiwemo adhabu ya kifo.

Oryem Nyeko ni mtafiti wa Human Rights watch upande wa Afrika na anasema, "ni muhimu kwa serikali ya Uganda kuweka wazi kwamba ukatili dhidi ya mtu yeyote haukubaliki bila ya kujali jinsia yake ama utambulisho wake wa kijinsia. Badala ya kuitisha sheria zinazolenga kutoa adhabu ya kifo, serikali ingejielekeza kutoa haki dhidi ya mauaji hayo."

Hofu dhidi ya watu wanaoshiriki vitendo vya jinsia moja imeongezeka kutoka kwa serikali ya Uganda, katika siku za hivi karibuni.

Uganda Entebbe | LGBT Pride Feier
Watu wakishiriki maandamano jijini Entebbe mwaka 2014 ya mapenzi ya jinsia mojaPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Vassie

Waziri wa usalama Elly Tumwine pia alinukuliwa mnamo Oktoba 3 kwamba watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja wanahusishwa na kundi la kigaidi.

Wasswa aliyekuwa akiishi mwenyewe alishambuliwa oktoba 4, ambapo watoto wa majirani waliukuta mlango wake ukiwa wazi majira ya alfajiri na kumkuta katika dimbwi la damu. Majirani walimuwahisha Wasswa hospitali ya Jinja, ambapo madaktari walimkuta akiwa hai, lakini wakabaini kwamba alishambuliwa na kitu cha ncha kali. Wasswa alifariki njiani wakati akikimbizwa hospitali ya Mulago jijini kampala.

Polisi wameanzisha uchunguzi na kubaini kifaa kilichotumika kumuua huku shahidi mmoja akielezea kumuona mwanaume mmoja nyumbani kwa Wasswa saa chache kabla ya kifo chake. Naibu mkurugenzi wa asasi inayotetea na kukuza haki za mapenzi ya jinisia moja nchini Uganda HRAPF, Edward Mwebaza, alisema Wasswa alikuwa shoga na wakati mwingine akijelezea kuwa mtu aliyebadili jinsia. Asasi hiyo imetoa wito kwa polisi kuchunguza uwezekano wa mauaji yaliyochochewa na chuki.

Mwebaza anasema mashoga watatu na wale waliobadili jinsia wameuawa nchini Uganda katika miezi ya hivi karibuni, katikati mwa ongezeko la kauli za chuki kutoka kwa wanasiasa dhidi ya jamii hiyo.

HRW