1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda: Mashoga walipeleka gazeti mahakamani

Saumu Ramadhani Yusuf10 Novemba 2010

Jamii ya mashoga nchi Uganda sasa imemua kulipeleka mahakani gazeti la Rolling Stone la nchini humo kwa kile wanachosema ni kuhatarishiwa maisha yao kutokana na gazeti hilo kuchapisha picha zao

https://p.dw.com/p/Q3gg
Uganda
UgandaPicha: DW

Gazeti la Rolling Stone lilianza kuchapishwa takriban miezi minne iliyopita lakini limepata umaarufu mkubwa nje na ndani ya Uganda kwa kuchapisha majina, picha na anuani za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Mapema mwezi huu (Novemba 2010) mahakama kuu nchini humo ilitoa agizo kwa gazeti hilo kukoma kufanya hivyo. Lakini bado jamii ya mashoga haijaepuka kuandamwa na gazeti hilo, kwani amri hiyo ya mahakama ilikuwa ya muda tu na Novemba 23 inatazamiwa kutoa uamuzi wake wa mwisho juu ya suala hilo.

Jaji Vincent Musoke Kibuuka alisema katika hukumu yake kwamba uchapishaji wa majina ya watu hao ni hatua inayokwenda kinyume na haki ya mtu kuweka siri mambo yake binafsi. Hata hivyo, uamuzi huo wa mahakama haujamshawishi mhariri mkuu wa gazeti hilo, Giles Muhame, ambaye anasema kwamba pindi muda wa amri ya mahakama ukimalizika na wakishinda kesi, kazi ya kuwaanika hadharani mashoga itaendelea kama kawaida.

"Amri ya mahakama ambayo inatuzuia kuchapisha habari zozote zinazoweza kusababisha mashoga kutambuliwa itaheshimiwa na gazeti, lakini watu wanabidi kufahamu kwamba amri hiyo ni ya muda tu hadi Novemba 23. Kesi kubwa zaidi inaanza Novemba 23, tutaipinga na tutawashinda. Amri iliyotolewa itashindwa. Na tutakapo washinda mahakamani basi tutaendelea kuwabainisha mbele ya macho ya jamii." Anasema Muhame.

Matamshi aina hiyo yamepeleka salamu za hofu kwa jamii nzima ya mashoga nchini Uganda. Stosh Mugisha ni mmoja wa wale wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja ana umri wa miaka 33. Kimaumbile ni mwanamke lakini yeye anajihisi kuwa mume na hata ana mpenzi wake wa kike. Kwa mujibu wa Mugisha, maisha yamebadilika ghafla tangu picha yake ilipochapishwa na gazeti hilo. Amelazimika kuihama nyumba yake na kwenda mahala kwengine kabisa kutokana na hofu ya kushambuliwa kwa kupigwa mawe.

"Nilikwenda dukani ambako mara nyingi mimi hununua sigara. Mwanamke aliniambia, mimi siwauzii mashoga sigara kwa hivyo ondoka haraka. Lakini nilipokuwa nakwenda kwangu, nilisikia watu wakinizungumza. Lakini mimi nikafunga maskio na nilipokuwa nakaribia kufika kwangu, nikaskia jiwe limerushwa. Nilipotazama nyuma kwenye lango, kweli watu walikuwa wakijaribu kunirushia mawe." Analalamika Mugisha.

Takribani watu wanne wameshashambuliwa kufuatia kuchapishwa kwa orodha ya kwanza ya majina ya watu hao wanaofanya mapenzi ya jinsia moja mnamo mwezi Agosti mwaka huu,kwa mujibu wa kundi la walio wachache la SMUG.

Hata hivyo, Muhame ameshikilia msimamo wake kwamba gazeti lake halikusudii kuhatarisha usalama wa mashiga hao, ambao ni raia kama raia wengine, isipokuwa mojawapo ya majukumu yake kama mwandishi ni kufichua maovu katika jamii na kwamba anabidi kuuambia ulimwengu kwamba maadili ya taifa zima na bara zima kwa jumla yako hatarini.

Anawashauri mashoga nchini mwake wasipoteze muda kwenda mahakamani, isipokuwa waachane tu na vitendo vyao ambavyo yeye anaona si vya maadili.

''Badala ya kwenda mahakamani kushtaki gazeti letu ambalo litawashinda katika kesi hii, nawashauri kukaa pamoja na gazeti hili ili wakubaliane kwamba watakoma kuwaingiza watoto katika mtandao wao wa mashoga na hapo ndipo gazeti hili litaacha kuchapisha picha zao.''

Bado ni mapema kusema ikiwa jamii ya mashoga itashinda vita vyake vya kujinusuru mahakamani, lakini kwenye mitaa ya nchi hii ya Afrika Mashariki ambayo ina uhafidhina wa kimila na kidini, bado mashoga wana safari refu ya kwenda kabla ya kukubalika kwenye jamii kama watu wa kawaida.

Mwandishi: Leyla Ndinda/Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo