1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa na Uturuki zalaumiana kuhusu mzozo wa Libya

Lilian Mtono
30 Januari 2020

Wakati rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiilaumu Uturuki kukiuka makubaliano ya kusimamisha uingiliaji wa nje kwenye mzozo wa Libya, Uturuki inailaumu Ufaransa kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu nchini humo. 

https://p.dw.com/p/3X0Ze
Emmanuel Macron Frankreich
Picha: picture-alliance/abaca/W. Jacques

Wakati rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiilaumu Uturuki kukiuka makubaliano ya kusimamisha uingiliaji wa nje kwenye mzozo wa Libya, baada ya kutuma meli za kivita na wanajeshi wa kukodi kuingia kwenye taifa hilo la Afrika Kaskazini, Uturuki kwa upande wake inailaumu Ufaransa kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu nchini humo. 

"Na hapa nataka pia kuzungumzia wasiwasi wangu kuhusu hatua za karibuni za Uturuki zinazotofautiana na dhamira ya rais Erdogan kwenye mkutano wa Berlin. Siku chache zilizopita tumeziona meli za Uturuki zikiongozana na wanajeshi wa kukodi wa Syria wakiingia kwenye ardhi ya Libya. Huu ni ukiukwaji mkubwa sana wa kile tulichokubaliana Berlin." alisema Macron.

Rais Emmanuel Macron amesema hayo baada ya mkutano na waziri mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis mjini Paris.

Mapema jana, jeshi la Uturuki lilisema kuna manowari zake nne na meli za kujaza mafuta katika eneo la katikati ya Mediterania, nje ya eneo la maji la Libya zinazosaidia operesheni za jumuiya ya kujihami ya Ulaya, NATO kwenye ukanda huo, wakati pia ikifanya shughuli zake za kuhakikisha usalama wa njia za biashara za majini.

Hatua hiyo inatokana na makubaliano ya shughuli za majini kati ya Uturuki na Libya yaliyofikiwa mwaka jana, ambayo yangeyawezesha mataifa hayo mawili kuufikia ukanda wa kiuchumi licha ya vikwazo kutoka Ugiriki, Misri na Cyprus, mataifa ambayo kijiografia yanakutana katikati ya Libya na Uturuki.  

Libyen Konflikt Symbolbild | eneral Haftar ARCHIV
Uturuki imeilaumu Ufaransa kwa kuwa chanzo cha mzozo wa Libya, na kutaka kuacha kumsaidia Khalifa HaftarPicha: AFP/A. Doma

Rais Emmanuel Macron ameyaelezea makubaliano hayo kama nyaraka zisizo halali na zisizokuwa na msingi wa kisheria ama hata kisiasa.

Uturuki yaitaka Ufaransa kuacha kumsaidia mbabe wa kivita Khalifa Haftar.

Huku Macron akitoa matamshi hayo, Uturuki nayo imejibu kwa kuilaumu Ufaransa kuwa ndio chanzo cha kukosekana kwa hali ya utulivu nchini Libya. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Uturuki Hami Aksoy amesema kwenye taarifa yake kwamba muhusika mkuu wa matatizo ya Libya tangu kuanza kwa mzozo mwaka 2011 ni Ufaransa.  

Amenukuliwa akisema sio siri tena kwamba Ufaransa imekuwa ikimpatia misaada isiyo na masharti mbabe wa kivita nchini Libya, Khalifa Haftar ili awe na maamuzi kuhusu masuala ya maliasili za taifa hilo, akisema Macron mara nyingine hujaribu kutengeneza ajenda kwa madai yanayovutia.

Kulingana na Aksoy, msaada wa Ufaransa pamoja na mataifa mengine wanaomsaidia Khaftar kijeshi kupambana na serikali aliyoiita ni halali, ilikuwa ni kitisho kikubwa zaidi dhidi ya uhuru na umoja wa taifa hilo.

Aliongeza kuwa iwapo Ufaransa inataka kushiriki kwenye maamuzi yaliyofikiwa Berlin, inatakiwa kwanza kuondoa msaada huo kwa Haftar.