Uchaguzi wa Burundi hauaminiki una mapungufu | Matukio ya Afrika | DW | 25.07.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Uchaguzi wa Burundi hauaminiki una mapungufu

Rais Barack Obama wa Marekani ameushutumu uchaguzi wa Burundi wa wiki hii kwamba ulikuwa hauaminiki wakati kiongozi wa chama kikuu cha upinzani ameyakataa matokeo ya uchaguzi huo na kutaka ufanyike uchaguzi mpya.

Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika mkutano na waandishi wa habari Nairobi.(25.07.2015)

Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika mkutano na waandishi wa habari Nairobi.(25.07.2015)

Kufuatia mazungumzo yake na Rais Uhuru Keyatta mjini Nairobi Kenya Jumamosi amesema wamelizungumzia suala la Burundi ambapo uchaguzi uliofanyika nchini humo ulikuwa sio wa kuaminika na wanatowa wito kwa serikali na upinzani kukutana kwa mazungumzo yatakayopelekea kupatikana na suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa nchi hiyo na kuepusha kupotea zaidi kwa maisha ya watu wasiokuwa na hatia.

Rais Piere Nkurunziza ameshinda muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi uliofanyika Jumanne ambao umesusiwa na upinzani. Wapinzani wanamashutumu kwa kukiuka katiba kutokana na kuwania kipindi kengine cha miaka mitano madarakani.

Tume ya uchaguzi imesema hapo Ijumaa kwamba rais huyo ambaye ametaja hukumu ya mahakama iliomruhusu kuwania tena urais amejizolea asilimia 73 ya kura.

Azma ya Nkurunziza kuwania muhula wa tatu imeitumbukiza Burundi katika mzozo mkubwa kabisa kuwahi kushuhudia tokea kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyochochewa chini ya misingi ya kikabila hapo mwaka 2005. Watu kadhaa wameuwawa katika maandamano yaliyodumu kwa wiki kadhaa na wengine zaidi ya 170,000 wamekimbilia katika makambi ya wakimbizi katika nchi za jirani.

Uchaguzi una mapungufu

Waandamanaji Bujumbura.

Waandamanaji Bujumbura.

Akitangaza uchaguzi huo kuwa na mapungufu makubwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema katika taarifa kwamba ni muhimu kwa serikali ya Burundi kuanza kujishughulisha kwa haraka katika mazingumzo ya maana na makini na viongozi wa upinzani na mashirika ya kiraia kufikia muafaka wa kusonga mbele kwa nchi hiyo.

Chama tawala cha CNDD-FDD kimetupilia mbali shutuma hizo za serikali ya Marekani kuhusu uchaguzi huo ambazo zilitolewa kabla ya hata ya uchaguzi wenyewe kuanza.Kiongozi wa chama hicho Pascal Nyabenda amesema kauli za serikali ya Marekani sio nzuri na ni kanusho kwa sheria zote za ubinaadamu ikimaanisha kwamba wananchi wa Burundi hawawezi kujitawala.

Mazungumzo yaliokuwa yakifanyika kwa siku kadhaa kati ya serikali,vyama vya upinzani, mashirika ya serikali na wawakilishi wengine yameshindwa kuutatuwa mzozo huo.

Uitishwe uchaguzi mpya

Agathon Rwasa kiongozi wa upinzani Burundi.

Agathon Rwasa kiongozi wa upinzani Burundi.

Kiongozi mkuu wa upinzani Agatho Rwasa hapo Jumamosi ameshutumu muhula wa tatu wa ushindi wa Nkurunziza na amedai kufanyika kwa uchaguzi mpya.

Rwasa ambaye amejipatia asilimia 18.9 ya kura licha ya kusema kwamba hakuweza kufanya vizuri kampeni yake amesema hangelipinga kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa iwapo dhamira ya msingi ya serikali hiyo itakuwa ni kuandaa uchaguzi huru na wa demokrasia.

Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika hazikupeleka waangalizi katika uchaguzi huo kwa sababu ya kile ilichosema mchakato huo mzima kuwa sio wa kuaminika.

Nchi jirani za Afrika Mashariki ambazo zilituma waangalizi katika uchaguzi huo zinasema kwa jumla umefanyika kwa utulivu hapo Jumanne lakini mchakato huo una mapungufu ya kanuni na viwango kuandaa uchaguzi huru, wa haki, amani,uwazi na wa kuaminika.

Imetaja masuala kama vile ya vurugu za kabla ya uchaguzi na mashaka ya usalama miongoni mwa wananchi,vikwazo dhidi ya vyombo vya habari na kususiwa kwa uchaguzi huo na vyama vya upinzani. Mataifa ya Afrika pia yametowa wito wa kufanyika kwa mazungumzo.

Upinzani pia umesusia uchaguzi wa bunge wa Juni 29 ambapo kwayo chama cha Nkurunziza cha FNDD-CNDD pia kilishinda pamoja na ule wa urais.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters/AFP

Mhariri : Isaac Gamba