1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Takaichi kuzungumza na Kim kuhusu utekaji wa raia wake

3 Novemba 2025

Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi ametuma ombi la kuzungumza na rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, kusawazisha mvutano wao wa muda mrefu kuhusu utekaji wa raia wa Japan uliofanywa na Pyongyang miongo iliyopita.

https://p.dw.com/p/530wR
Japan Tokio 2025 | Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi
Takaichi kuzungumza na Kim kuhusu utekaji wa raia wake Picha: Kim Kyung-Hoon/REUTERS

Takaichi amesema ili kujenga uhusiano ulio wa wazi na wakuaminiana, ni lazima akutane ana kwa ana na Kim Jong Un, kujadili suala hilo. Bado utawala wa Kim haujasema chochote kuhusu ombi hilo.

Viongozi wa zamani wamejaribu kuwa na mazungumzo na Kim kuhusu utekaji huo lakini juhudi zao hazikufua dafu.

Baada ya miaka mingi ya kukanusha madai hayo, mwaka 2002, Korea Kaskazini ilisema maafisa wake waliwateka nyara raia  13 wa Japan miaka ya 70 na 80, waliotumika kuwapa mafunzo ya lugha na tamaduni za kijapani wapelelezi wa Korea Kaskazini.

Hata hivyo Japan inaamini raia wake waliotekwa wanafikia 17 huku maafisa wengine wakisema idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi.