1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Taiwan 'itatetea maadili ya uhuru na demokrasia"

23 Mei 2024

China imeizingira Taiwan kwa vikosi vya majini na ndege za kivita katika luteka za kijeshi, ikiapa kwamba damu ya vikosi vya uhuru kwenye kisiwa hicho kinachojitawala itatiririka.

https://p.dw.com/p/4gC3J
Ufuatiliaji wa Wizara ya Ulinzi ya Taiwan
Mabaharia wa jeshi la wanamaji wa Taiwan wakiwa wamesimama kwenye meli ya kivita ya majini wakati wa mazoezi ya Wanamaji huko Kaohsiung, Taiwan.Picha: Ritchie B. Tongo/dpa/picture alliance

Luteka hizo za siku mbili ni sehemu ya kampeni inayoongezeka ya vitisho vya China kufanya mfululizo wa operesheni kubwa za kijeshi karibu na Taiwan katika miaka ya hivi karibuni.

Hatua hii mpya inajiri baada yaLai Ching-te kuapishwa kama rais mpya wa Taiwan wiki hii huku China ikiikosoa hotuba yake baada ya kuapishwa na kuitaja kama "ungamo la uhuru".

Soma pia: Taiwan yaripoti shughuli za kijeshi za China baada ya Blinken kuondoka Beijing

Wakati luteka hizo zikiendelea, jeshi la China limesema litatoa "adhabu kali kwa vitendo vya kujitenga vinavyofanywa na vikosi vya uhuru vya Taiwan."

Msemaji wa wizara ya mambo ya njewa China, Wang Wenbin, alitoa onyo kali kwa kutumia lugha yenye maneno makali na vitisho.

"Vitendo vyote vya kujitenga kwa Taiwan vitakutana na shambulio la mbele la watu bilioni 1.4 wa China, vikosi vyote vya uhuru wa Taiwan vitaachwa vikiwa vimevunjwa vichwa na damu inatiririka baada ya kugongana dhidi ya mwelekeo wa kihistoria wa China kufikia umoja kamili."

Taiwan itajilinda na kutetea demokrasia yake

Taiwan | Rais Lai Ching-te atembelea kituo cha kijeshi huko Taoyuan
Rais wa Taiwan Lai Ching-te akipiga picha pamoja na wanajeshi wakati wa ziara yake katika kambi ya kijeshi huko Taoyuan.Picha: Ann Wang/REUTERS

Hata hivyo Taiwan ilijibu uchokozi wa China kwa kupeleka vikosi vya anga, ardhini na baharini, huku wizara ya ulinzi ya kisiwa hicho ikiapa "kutetea uhuru" wake.

Katika taarifa, msemaji wa ofisi ya rais, Karen Kuo, amesema inasikitisha kuona China ikitumia tabia za kijeshi za uchochezi na za pande moja zinazotishia demokrasia na uhuru wa Taiwan pamoja na amani na utulivu wa kikanda.

Soma pia:Taiwan yamtaka Scholz aionye China dhidi ya uvamizi wa kijeshi 

Kuo ameongeza kusema wakati kisiwa hicho kinachojitawala kinapokabiliwa na vitisho na changamoto kutoka nje, kitaendelea kutetea demokrasia yake.

Rais Lai Ching-te ameahidi kusimama katika mstari wa mbele wa vita pamoja na wanajeshi wa nchi hiyo kulinda usalama wa kitaifa wa Taiwan bila ya kutaja waziwazi luteka za kijeshi za China.

Beijing, ambayo iligawanyika na Taipei mwishoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka 75 iliyopita, inakichukulia kisiwa hicho kama eneo lake na kwamba ni lazima hatimaye liunganishwe.

Mara kwa mara China imekuwa ikiongeza shinikizo kwa kisiwa chenye watu milioni 23, kinachojitawala kidemkorasia, na kuibua wasiwasi juu ya uwezekano wa uvamizi.

 

/AFP