Syria yakubali muda wa kusimamisha ghasia | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Syria yakubali muda wa kusimamisha ghasia

Syria imekubali tarehe 10 Aprili kama muda wa mwisho kuanza kutekeleza mpango wa amani uliopendekezwa na mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Kofi Annan.

Rais wa Syria, Bashar al Assad

Rais wa Syria, Bashar al Assad

Bwana Kofi Annan ametoa taarifa juu ya ridhaa ya serikali ya Syria kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York kupitia njia ya Video yeye akiwa mjini Geneva. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Susan Rice ameliambia Baraza la Usalama kuwa Annan amesema kwamba Syria imekubali kuwa ifikapo tarehe 10 April itakuwa imeondoa wanajeshi wake na zana nzito nzito za kijeshi kutoka miji yenye harakati za upinzani.

Ujumbe wa kulinda amani

Kofi Annan, mjumbe wa kimataifa nchini Syria

Kofi Annan, mjumbe wa kimataifa nchini Syria

Annan pia ameutaka Umoja wa Mataifa kuanza kufikiria ujumbe utakaosimamia amani nchini Syria. Balozi wa Syria kwenye umoja wa Mataifa, Bashar Jaafari amethibitisha ridhaa ya nchi yake kuheshimu muda huo.

''Bwana Kofi Annan amekuwa akiwasiliana na maafisa wa serikali yetu mara kwa mara, na pande zote zimepata muafaka wa kufanya kazi pamoja, kutafuta njia nzuri za kusimamia utekelezwaji wa mpango wa amani wenye vipengele sita kwa kuheshimu uhuru wa Syria''. Alisema Jafari.

Lakini ridhaa ya Syria imepokelewa kwa mashaka na baadhi ya nchi, kama alivyoeleza Susan Rice, balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa.

Mashaka juu ya ''nia njema''

Susan Rice, balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa

Susan Rice, balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa

''Baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama wameeleza wasi wasi wao, wakisema Syria isje ikatumia siku chache zinazosalia kuzidisha ukandamizaji. Na wana mashaka juu ya wema wa nia ya Syria juu ya mpango huo. Lakini kwa ujumla wanachama wa baraza la usalama wameelezea utashi wao kutafakari pendekezo la bwana Annan kuweka ujumbe wa kulinda amani, iwapo kweli ghasia zitasimamishwa.'' Alisema bi Rice.

Urusi ambayo siku zilizopita ilitaka serikali ya Syria na waasi wasimamishe matumizi ya nguvu kwa wakati mmoja, sasa inakubaliana na mpango wa Kofi Annan unaoitaka serikali kuchukua hatua ya kwanza.

Wanadiplomasia wamesema kwamba mpango wa amani wa Kofi Annan wenye vipengele sita, unataka usitishwaji kamili wa ghasia zote katika masaa 48 baada ya tarehe 10 April. Mbali na na kusimamishwa kwa vurugu, mpango wa Annan unahimiza mazungumzo ya kisiasa yatakayoongozwa na wasyria wenyewe, haki ya watu kuandamana, na kufunguliwa kwa watu waliwekwa kizuizini kimabavu.

30 zaida wafa katika ghasia

Jeshi la Syria limeripotiwa kusaka wapinzani katika miji yenye uasi

Jeshi la Syria limeripotiwa kusaka wapinzani katika miji yenye uasi

Wakati hayo yakijiri, kuna ripoti za kuuawa kwa watu wengine zaidi ya 30 katika ghasia ndani ya Syria, na mkuu wa shirika la Msalanba Mwekundu Jakob Kellenberger ameanzisha ujumbe mpya wa kibinadamu nchini Syria, wa tatu tangu kuanza kwa machafuko mwaka mmoja uliopita. Ripoti hizo zilisema vikosi vya serikali vimeingia kwa vifaru katika miji yenye uasi, na kuwakamata wanaharakati na pia kuchoma na kubomoa nyumba zao.

Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London, jana limesema kuwa watu 10,108 wamekwishauawa katika mgogoro wa Syria.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE/AP

Mhariri:Yusuf Saumu

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com