Sudan yadaiwa kuwaua Wanubi | Matukio ya Afrika | DW | 14.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Sudan yadaiwa kuwaua Wanubi

Jeshi la Sudan, likisaidiwa na wapiganaji wanaoungwa mkono na serikali, linatuhumiwa kuendesha kampeni ya mauaji ya watu wengi huko Kordofan Kusini, likiwalenga hasa watu wa kabila la kiasili la Nuba.

Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan

Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan

Ripoti ya kundi la kutetea haki za binaadamu nchini Sudan la SDGP, iliyotolewa jana (13.06.2011) imevikosoa vikosi vya serikali kwa uhalifu kadhaa na ukiukaji wa haki za binaadamu unaofanywa dhidi ya raia kwenye eneo hilo lililopo kwenye jimbo la milima ya Nuba.

Kundi hilo limesema, wiki iliyopita jeshi la Sudan, likisaidiwa na vikosi vya jeshi la wananchi, lilifanya ukatili, ikiwemo mauaji, kuwakamata watu hovyo, utesaji, kuchoma mali kwa makusudi pamoja na kuharibu miundombinu na kuchoma moto makanisa, hasa katika miji ya Kadugli na Deleng.

Maafisa wa serikali hawakupatikana mara moja kujibu shutuma hizo.

Mapigano kati ya jeshi la Sudan ya Kaskazini na jeshi la SPLA la Kusini yalizuka kwa mara ya kwanza tarehe 5 Juni. Wasiwasi umeendelea kuongezeka miongoni mwa raia kutokana na mashambulio ya anga kwenye eneo hilo, ambalo lilikuwa ngome kuu ya waasi, ambako watu wa kabila la Nuba walipigana upande wa SPLA wakati wa mapigano makali ya miaka 22 na serikali ya Sudan.

Viongozi wa Kiislamu Kenya wataka adhabu ya kifo kwa mashoga

Rais Mwai Kibaki wa Kenya (kulia)

Rais Mwai Kibaki wa Kenya (kulia)

Viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Kenya wameitaka serikali kuanzisha adhabu ya kifo dhidi ya mashoga na kususia shughuli zao.

Akinukuliwa na gazeti la Daily Nation, Sheikh Mohammed Khalifa wa Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini Kenya, amesema kwa mujibu wa dini ya Kiislamu, kifo ndio adhabu pekee dhidi ya watu wa aina hiyo kama inavyofanyika China na Iran.

Amesema wamewaomba Wakenya kususia biashara zinazofanywa na kumilikiwa na watu wa aina hiyo na kuonyesha wazi wazi kuwatenga na kuwabagua kama njia ya kuwafanya waachane na tabia hiyo. Sheikh Khalifa ameongeza kusema kuwa watu hao wanakiuka haki na hawatakiwi kukubalika miongoni mwa jamii.

Matamshi hayo ameyatoa katika warsha ya kuzungumzia unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa dhidi ya watoto wa kiume ambayo imehudhuriwa na zaidi ya walimu 150 wa madrassa za Kiislamu. Ushoga ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi za Afrika.

Vumbi la Volkano laparaganya safari za ndege Afrika Mashariki

Ndege ikiruka juu ya Mlima wa Volkano iliyokufa

Ndege ikiruka juu ya Mlima wa Volkano iliyokufa

Wingu la vumbi linalotokana na mripuko wa Volkano uliotokea Eritrea, leo limesababisha mpagaranyiko katika safari za ndege huko Afrika Mashariki.

Hailaye Gebretsadik, meneja mkuu wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Bole, mjini Addis Ababa, Ethiopia, amesema safari za ndege za usiku za Shirika la Kijerumani la Lufthansa kutokea Frankfurt na ndege ya Shirika la Umoja wa Falme za Kiarabu, Emirates, kutoka Entebbe, Uganda, zilifutwa.

Mripuko wa Volkano wa Dubi ulitokea Jumapili usiku baada ya kutokea mlolongo wa mitetemeko midogo. Mripuko huo ni wa mwanzo tangu miaka 150 iliyopita. Safari za ndege kutoka na kwenda Addis Ababa hazijaathirika.

Kwa mujibu wa idara ya utabiri wa hali ya hewa ya Israel, wimbi hilo la vumbi linaelekea upande wa Saudi Arabia na Jordan.

Zambia kujenga kinu kipya cha umeme

Msitu wa Miombo nchini Zambia

Msitu wa Miombo nchini Zambia

Shirila la nishati la Copperbelt Energy linalotoa umeme kwa ajili ya migodi ya Zambia, limesema leo kwamba litajenga mtambo wa umeme wa Megawati 40 kutoka nguvu za maji kwenye eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo lenye utajiri wa madini ya shaba.

Kampuni hiyo itaanza kujenga bwawa hapo mwakani lenye gharama ya Euro milioni 118 na litamalizika mwaka 2015.

Mkurugenzi wa mradi huo, Aaron Botha, aliwaambia waandishi wa habari kwamba kampuni hiyo sasa inajaribu kuwapatia makaazi mapya wanavijiji 500 ili bwawa hilo lijengwe katika wilaya ya Kabompo, kaskazini-magharibi mwa nchi, kilomita 850 kutoka mji mkuu, Lusaka.

Alisema wanavijiji wamekubali kuhamishwa na watajengewa makaazi yaliyo bora zaidi.

Maharamia waichia meli

Miongoni mwa meli zilizowahi kutekwa na maharamia wa Kisomali

Miongoni mwa meli zilizowahi kutekwa na maharamia wa Kisomali

Maharamia wa Kisomali wameiachia meli ya mizigo ya Misri, MV Suez, baada ya kupokea fidia ya dola milioni 2.1. Hayo ni kwa mujibu wa duru za maharamia na makampuni ya misafara ya meli.

Meli hiyo inayosafiri chini ya bendera ya Panama na inayosimamiwa na kampuni ya Misri mjini Port Said, ilikamatwa mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka jana ikiwa na mabaharia 23.

Haramia kwa jina la Ali ameliambia shirika la habari la Reuters jana kwamba wao wamepokea fedha hizo na wameiachia huru meli hiyo.

Andrew Mwangura, mhariri wa safari za bahari wa jarida la Somalia Report, alihakikisha kutoka bandari ya Mombasa kwamba meli hiyo imeachiwa na sasa inasafiri kutoka eneo la bahari ya Somalia.

Mwandishi: Grace Kabogo
Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com