1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Upinzani wadai waandamanaji 9 wameuwawa

Zainab Aziz
21 Desemba 2018

Msemaji wa upinzani asema idadi ya watu waliokufa imeongezeka na kufikia watu tisa ncini Sudan hata hivyo,taarifa za vyombo vya habari vya Sudan vinaweka idadi ya vifo hivyo kuwa ni watu sita.

https://p.dw.com/p/3AVMG
Sudan Unruhen in Atbara
Picha: Reuters/E. Siddig

Watu hao walikuwa wanashiriki kwenye maandamano ya kupinga kuongezeka kwa bei za bidhaa na chakula nchini humo hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa chama cha upinzani cha UMMA, Mohamed Zaki alipozungumza kwa njia ya simu na shirika la habari la nchini Ujerumani la dpa. Wakati huo huo amri ya kutotoka nje imetolewa katika mikoa miwili katika eneo la Mashariki la al-Gadarif na lile la kaskazini la Atbara.

Hasira ya wananchi wa Sudan imekuwa ikiongezeka kutokana na matatizo ya kiuchumi pamoja na kupanda mara mbili kwa gharama ya chakula kama mkate katika mwaka huu na pia watu kuwekewa viwango vya kutoa fedha benki kwa asilimia 69.  Mfumuko wa bei nchini Sudan ni wa juu zaidi  ulimwenguni.

Kiongozi maarufu wa chama cha upinzani cha UMMA cha nchini Sudan Sadiq al-Mahdi aliyerejea nchini humo siku ya Jumatano baada ya kuwa uhamishoni kwa karibu mwaka mmoja amesema serikali imeshindwa na kusababisha uchumi wa Sudan kuzorota hivyp basi ametoa mwito wa kufanyika utaratibu wa utawala wa mpito wa kidemokrasia nchini humo.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir
Rais wa Sudan Omar al-BashirPicha: Reuters/M. Abdallah

Waziri wa Habari wa Sudan Osman Muhammad Bilal amekiri kwamba polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi ili kuvunja maandamano hayo. Bilal katika kuitetea serikali amesema wanachunguza taarifa za vifo hivyo. Wakati huo huo serikali ya Sudan imesema inafanya kila inachoweza kukabiliana na uhaba wa mahitaji ya msingi kama chakula na huduma nyingine, lakini haitasita vilevile kukabiliana na mtu yeyote anayevunja sheria.

Msemaji wa serikali Bishara Gomaa pia alikiri kutokea vifo wakati wa maandamano ya siku mbili zilizopita, lakini hakutoa maelezo zaidi. Hasira na chuki kubwa vimekuwa vikipanda kwa wiki kadhaa nchini Sudan kufuatia kushuka haraka kwa hali ya uchumi.

Maandamano kama hayo yalifanyika mwezi Januari juu ya suala hilo hilo, na polisi walitumia gesi ya machozi kuwatawanya mamia ya waandamanaji katika mji mkuu wa Khartoum,mwishoni mwa mwaka 2016 baada ya serikali kukata ruzuku ya mafuta.

Uchumi wa nchihiyo tajiri yenye mafuta uliathirika vibaya wakati ilipojigawa na kuundwa Sudan ya pili ambayo ni Sudan Kusini mnamo mwaka 2011. Mpaka sasa serikali ya Sudan ya rais Omar al-Bashir inapambana na makundi kadhaa ya waasi.

Mwaandishi: Zainab Aziz/AP/DPA/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef