Shirika la DRC laonya wimbi jipya la wakimbizi
16 Aprili 2026
Vita, migogoro, vurugu na mateso vinatarajiwa kuwafanya watu milioni 4.2 kuyakimbia makazi yao ifikapo mwisho wa mwaka 2027, bila kujumuisha wale wanaoathiriwa na vita vya Mashariki ya Kati.
Haya ni kwa mujibu wa makadirio mapya ya shirika la misaada la Denmark, Baraza la Wakimbizi la Denmark (DRC), ambayo yanaonyesha ongezeko kubwa la watu wanaokimbia vita na ukatili duniani.
Katibu Mkuu wa shirika hilo, Charlotte Slente, anasema makadirio hayo hayajumuishi walioathiriwa na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati, ambako mapigano mapya yanaendelea kusababisha maelfu kuhama makazi yao.
Baraza la Wakimbizi la Denmark linaongeza kuwa tayari kuna zaidi ya watu milioni 117 waliotawanywa duniani, na hali inazidi kuwa mbaya kutokana na kupungua kwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu.
Katika nchi tano zilizokuwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi mwaka 2025—Ukraine, Myanmar, Sudan Kusini, Nigeria na Mali—ufadhili wa juhudi za amani ulipungua kwa wastani wa asilimia 23 mwaka 2024.