1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Shambulio la Urusi Kharkiv laua watu 10

7 Machi 2026

Shambulio la kombora la Urusi limepiga jengo la makazi mjini Kharkiv na kuua watu 10 wakiwemo watoto wawili. Rais Zelenskiy ameomba majibu ya kimataifa huku mashambulizi ya makombora na droni yakiendelea kote Ukraine.

https://p.dw.com/p/59zOa
Ukraine, Kharkiv 2026 | Vikosi vya uokoaji baada ya shambulio la kombora la Urusi kwenye jengo la makazi
Waokoaji wakifanya kazi katika eneo la jengo la makazi lililopigwa na shambulio la kombora la Urusi, wakati wa mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine, mjini Kharkiv.Picha: Vyacheslav Madiyevskyy/REUTERS

Watoto wawili ni miongoni mwa watu wasiopungua kumi waliouawa siku ya Jumamosi baada ya kombora la Urusi kupiga jengo la makazi la ghorofa tano katika mji wa Kharkiv, mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, maafisa wamesema. Watu wengine 16 walijeruhiwa katika shambulio hilo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alilaani mashambulizi hayo na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya Urusi.

Alisema Urusi ilishambulia Ukraine usiku kwa makombora 29 na droni 480, zikilenga vituo vya nishati katika mji mkuu Kyiv na maeneo mengine ya katikati ya nchi.

Kwa mujibu wa takwimu za awali, mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine iliangusha makombora 19 na droni 453.

Hata hivyo, makombora tisa na droni 26 zilifanikiwa kulenga maeneo 22 tofauti nchini humo.

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

Uokoaji waendelea katika kifusi Kharkiv

Katika mji wa Kharkiv kaskazini mashariki mwa Ukraine, wahudumu wa dharura waliendelea kutafuta manusura chini ya kifusi cha jengo lililoharibiwa.

Miongoni mwa waliouawa kulikuwa na mwalimu wa shule ya msingi na mwanawe aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la pili, ambao walifariki ndani ya nyumba yao.

Mwanafunzi mwingine wa darasa la nane pia aliuawa pamoja na mama yake, kwa mujibu wa meya wa mji huo Ihor Terekhov.

Ofisi ya mwendesha mashtaka ya mkoa ilisema jengo hilo lilipigwa na kombora jipya la Urusi linalojulikana kama Izdeliye-30.

Ripoti za Ukraine zinasema silaha hiyo mpya ya kurushwa kutoka angani ina uwezo wa kufika umbali wa kilomita 1,500 na ina mfumo mpya wa urambazaji wa satelaiti unaoweza kustahimili kuingiliwa.

Miundombinu yashambuliwa maeneo mengine

Katika eneo la Kyiv, mamlaka za mitaa ziliripoti uharibifu uliosababishwa na mabaki ya makombora katika wilaya tatu tofauti.

Katika mkoa wa kusini wa Odesa, wazima moto 80 walitumwa kukabiliana na moto mkubwa katika miundombinu baada ya mashambulizi ya droni kadhaa.

Shirika la reli la Ukraine Ukrzaliznytsia lilisema uharibifu wa miundombinu ya reli ulilazimisha mabadiliko ya baadhi ya njia za usafiri katika sehemu ya kati-magharibi ya nchi.

Kutibu majeraha yaliosababishwa na vita Ukraine

Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema mashambulizi ya usiku yalilenga viwanda vya kijeshi vya Ukraine, vituo vya nishati na kambi za jeshi la anga.

Zelenskyy alisema washirika wa Ukraine wanapaswa kujibu mashambulizi hayo makali dhidi ya raia.

Droni za Iran zatumika sana katika vita

"Lazima kuwe na majibu kutoka kwa washirika kwa mashambulizi haya ya kikatili dhidi ya maisha,” Zelenskyy alisema katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X.

Urusi imekuwa ikitumia kwa wingi droni zilizobuniwa na Iran kushambulia Ukraine tangu ilipoanzisha uvamizi wake zaidi ya miaka minne iliyopita.

Maelfu ya droni hizo zimezinduliwa dhidi ya Ukraine, huku Urusi pia ikianzisha uzalishaji mkubwa wa ndani wa silaha hizo.

Katika baadhi ya nyusiku, mamia ya droni zimekuwa zikishambulia Ukraine kwa wakati mmoja, idadi inayozidi mashambulizi yaliyofanyika katika miezi kadhaa ya mwaka 2024.

Wakati huo huo, Iran pia imetumia droni hizo hizo aina ya Shahed kushambulia nchi za Mashariki ya Kati kujibu mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel.

NATO ni nini?

Vita Mashariki ya Kati vyageuza umakini wa dunia

Zelenskiy alisema Ukraine pia imepokea ombi kutoka Marekani la kusaidia kulinda nchi za Mashariki ya Kati dhidi ya droni za Iran.

Alisema tayari ameagiza vifaa na wataalamu wa Ukraine kusaidia katika juhudi hizo.

Wakati huo huo, vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vimeelekeza umakini wa kimataifa mbali na vita vya Ukraine.

Mzozo huo mpya pia umesababisha kuahirishwa kwa duru mpya ya mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine iliyokuwa ipatanishwe na Marekani wiki hii.

Vita vya Ukraine vinaendelea kuwa mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.