1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sekta ya usafirishaji yazidi kuathirika na Corona

Lilian Mtono
5 Machi 2020

Umoja wa Falme za Kiarabu umewaonya raia wake pamoja na wageni waishio nchini humo kutosafiri nje ya nchi katika wakati ambapo mripuko wa virusi vya Corona ukizidi kusamba.

https://p.dw.com/p/3YtpE
Emirates Airbus A380 Flugzeug
Picha: picture-alliance /M. Mainka

Hili likiwa ni onyo kali kwa taifa hilo ambalo linamiliki mashirika makubwa mawili ya ndege yanayosafiri masafa marefu  zaidi duniani ya Etihad na Emirates. 

Onyo hilo la wizara ya afya na ulinzi wa jamii linatolewa wakati mji mkuu wa Umoja huo wa Falme za Kiarabu Abu Dhabi ukiwa umewaweka karantini raia wa kigeni 215 ambao iliwaondoa kutoka Hubei nchini China ambako kumeathirika zaidi na ambako ni kitovu cha mripuko wa Corona. Raia hao ni pamoja na wanaotoka Misri, Sudan na Yemen.

Uwanja mkubwa na wenye shughuli nyingi mno wa ndege wa kimataifa wa Dubai ambao ni makao ya ndege za Emirates, unaomilikiwa na serikali unapatikana nchini humo lakini pia Abu Dhabi ambako kuna shirika la ndege la Etihad ambalo pia ni la serikali. Kwa pamoja mashirika hayo yamewataka wafanyakazi wake kwenda likizo, kutokana na kupungua kwa idadi ya wasafiri kufuatia mripuko huo.

Kumeripotiwa visa 3,150 hadi sasa vya Corona kote Mashariki ya Kati. Mamlaka kwenye eneo hilo zinasema virusi hivyo vimewaua takriban watu 92 katika wakati ambapo kumethibitishwa visa 2,922. Iran na Italia ndio mataifa yenye idadi kubwa ya vifo nje ya China vilivyosababishwa na virusi hivyo.

Kolumbien Juan Manuel Santos Interview in Bogota
Rais wa zamani wa Colombia, amehimiza ushirikiano na utoaji taarifa kamili katika kupambana na janga la Corona.Picha: Reuters/C. Julio Martinez

Kwenye kongamano la tisa la kimataifa la mawasiliano mjini Sharjah, Umoja wa Falme za Kiarabu, rais wa zamani wa Colombia Juan Manuel Santos miongoni mwa watu wengine maarufu kwenye kongamano hilo waliozungumzia janga hilo ameelezea uzoefu wake wa kukabiliana na  magonjwa ya miripuko, akiangazia enzi ya utawala wake na namna alivyopambana na mripuko wa maradhi ya homa ya Chikungunya 

"Pendekezo langu kwa serikali yoyote ni kutolidharau tatizo, na usijaribu kuficha ukweli, usidanganye maafisa wa afya na wataalamu, ruhusu taarifa nyingi iwezekanavyo. Ninachotumai ni kwamba jambo ambalo tunapitia linatufumbua macho yetu kwa ulimwengu kufahamu umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa. " amesema Santos

Korea Kusini imeripoti kesi 322 zaidi mpya za virusi hivyo vya Corona hii leo hii ikiwa ni kulingana na taasisi ya kudhibiti na kuzuia magonjwa, CDCP na idadi jumla sasa kufikia wagonjwa 6,088 baada ya kesi nyingine mpya kuripotiwa mapema leo.

Huko Indonesia wizara ya mambo ya kigeni imesema itawazuia kuingia na kupitia nchini humo wageni wanaotokea mataifa yaliyoathiriwa pakubwa na Corona kama Italia, Iran na Korea Kusini kuanzia Machi 8.

Nchini Ujerumani, taasisi ya afya ya umma ya Robert Koch imesema hii leo kwamba kumethibitishwa visa 109 katika kipindi cha siku moja, huku jimbo lililoathiriwa zaidi likiwa ni la North Rhine Westphalia, lenye visa 175. Kwa ujumla watu 349 wamethibitika kuwa na virusi hivyo nchini Ujerumani

Mashirika: RTRE