1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yaruhusu wahouthi walioumia kupelekwa Oman

13 Novemba 2018

Kikosi cha muungano wa kijeshi kinachoongozwa na Saudi Arabia kimetoa ruhsa ya waasi walioumizwa vitani kusafirishwa nchini Omna kutibiwa,hii ikiwa ni hatua ya kwanza inayotowa matumaini ya kufanyika mazungumzo

https://p.dw.com/p/38B8E

UN-Menschenrechtsrat
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Uamuzi wa kikosi cha muungano kinachoongozwa na Saudi Arabia katika mapambano dhidi ya waasi wa Kihouthi huko Yemen umekuja baada ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Uingerea Jeremy Hunt katika eneo hilo. Suala la kuhamishwa watu walioumia kutoka Yemen lilikuwa kizingiti kikuu katika mazungumzo ya awali ya amani na hatua ya hivi sasa iliyochukuliwa na kikosi hicho inaweza kufungua njia ya kuanza mazungumzo mapya.Waziri wa Hunt amezungumza na waandishi wa habari na kuthibitisha juu ya kilichoamuliwa na muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.

"Kitu kimoja ambacho ni habari nzuri ni kwamba leo Wasaudi wamenithibitishia kwamba wako tayari kuruhusu kuhamishwa wapiganaji 50 wakihouthi waliojeruhiwa ili wapelekwe kutibiwa nchini Oman, kukiweko masharto kuhusu nani watasafiri nao. Hii ni hatua muhimu sana kwasababu hili ni suala ambalo siku zote limekuwa ndio sharti mojawapo lililokuwa linatolewa na wahouthi ili washiriki kwenye mazungumzo ya amani ambayo yamepangwa kufanyika mwishoni mwa Novemba,ikiwa hatua hii itafungua njia hiyo inamaana kwamba kuna matumaini ya mazungumzo hayo kufanyika na hilo litakuwa muhimu.''

Jemen Hodeida Regierungstruppen rücken vor
Picha: Getty Images/AFP

Muungano huo wa kijeshi pia unaruhusu sasa Umoja wa Mataifa kusimamia shughuli nzima ya kuondolewa waasi hao wakihouthi wakiwemo wapiganaji na kupelekwa nchini Oman kabla ya duru nyingine ya mazungumzo iliyopendekezwa kuanza baadae mwezi huu. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Hunt alianza ziara yake Jumatatu iliyompeleka Riyadh na Abudhabi ambako alikutana na mfalme Salman na mwanamfalme Mohammad bin Salman sambamba na viongozi wengine  kutoka Umoja wa falme za kiarabu na Yemen.

Ziara yake hiyo ilikuwa na lengo la kuimarisha uungwaji mkono wa juhudi za Umoja wa Mataifa za kutaka kuumaliza mgogoro wa Yemen ambao umeshadumu kwa takriban miaka minne.Kadhalika lengo lake lilikuwa pia kuishinikiza Saudi Arabia juu ya mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi. Taarifa pia zinasema hali ya utulivu leo hii imeonekana katika mji wa bandari wa Hodeida kufuatia ziara hiyo ya kidiplomasia ya waziri wa mambo ya nje wa Uingereza.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Iddi SseSsanga

    

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW