1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana kwa makombora

8 Oktoba 2025

Ukraine na Urusi zimeshambuliana usiku wa kuamkia Jumatano 08.10.2025 ambapo takriban watu watano waliuawa.

https://p.dw.com/p/51eYQ
Urusi Belgorod | Mashambulizi ya droni ya Ukraine
Maafisa wa kikosi cha zimamoto wakipambana kuuzima moto kwenye gari inayoungua katika eneo la Belgorod nchini Urusi baada ya mashambulizi ya droni kutoka UkrainePicha: Governor of Belgorod Region Vyacheslav Gladkov via Telegram/via REUTERS

Kwa mujibu wa gavana wa mkoa wa Belgorod nchini Urusi, watu watatu wameuawa katika mashambulizi ya makombora kwenye kijiji cha Maslova Pristan, kilicho mpakani kati ya Urusi na Ukraine.

Gavana Vyacheslav Gladkov, amesema makombora ya Ukraine yamesababisha hasara kwenye kituo cha kijamii na amechapisha picha zinazoonyesha uharibifu katika sehemu ya usoni ya jumba la michezo. Gavana huyo wa mkoa wa Belgorod amesema mtu mmoja amejeruhiwa na kwamba huenda watu wengine wakawa wamefukiwa chini ya kifusi.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasemaje?

Wakati huo huo, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imezidungua droni 53 za Ukraine usiku wa kuamkia Jumatano, na nyingi zimeangushwa katika eneo la Belgorod, ambalo hulengwa mara kwa mara na mashambulizi kutoka Ukraine.

Kwa upande mwingine mashambulizi ya Urusi yaliulenga mji wa Kherson wa kusini mwa Ukraine na familia ya mume na mkewe wameuawa kwenye mashambulizi hayo ya kujibizana. Gavana wa eneo hilo Oleksandr Prokudin, amesema mwanamke mwenye umri wa miaka 62 na mwanamume ambaye bado hajatambuliwa wamejeruhiwa vibaya kwenye mashambulizi ya Urusi. 

Ukraine | Mashambulizi katika mji wa Kherson
Jengo lililoshambuliwa na droni za Urusi katika mji wa Kherson nchini UkrainePicha: Kherson Regional Military Administration/AP/dpa/picture alliance

Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi ilirusha takriban droni 183 katika eneo la Kherson nchini Ukraine kuanzia siku ya Jumanne jioni hadi mapema alfajiri ya Jumatano.

Lazima Ulaya iimarishe ulinzi wake

Huku hayo yakiendelea Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, amesisitiza kwamba lazima Ulaya iimarishe ulinzi wake ili kuweza kukabiliana na pia kuvizuia vita vya Urusi inayotumia mbinu tofauti tofauti katika mkakati wake wa vita. Von der Leyen ameyasema hayo baada ya msururu wa matukio ya uvamizi wa droni kwenye anga za baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya ya Umoja wa Ulaya, mashambulizi ya mtandaoni na pia uharibifu wa nyaya za chini ya bahari.

Von der Leyen, kwenye hotuba yake katika Bunge la Umoja wa Ulaya  amewaambia wabunge wa bunge hilo kwamba matukio haya ni kampeni iliyopangwa kwa uthabiti na inaendelea kupanuka huku wale ambao wana mashaka na kinachotokea bado wakiwa wanaendelea kukana.

Vyanzo: AFP/RTRE/DPA