Rotich na Thugge wakanusha mashtaka ya ufujaji fedha | Matukio ya Afrika | DW | 23.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Rotich na Thugge wakanusha mashtaka ya ufujaji fedha

Waziri wa Fedha wa Kenya Henry Rotich na katibu wake Thugge Kamau wamekanusha mashtaka ya ufujaji fedha za mabwawa mawili. wawili hao na maafisa wengine wanasemekana kushirikiana kufuja shilingi bilioni 17.

Rotich, Thugge na maafisa wengine wakuu serikalini walikaa kimya  kizimbani wakati wakisomewa mashtaka ya kuongeza thamani ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer kwa shilingi bilioni 17 katika mahakama ya Milimani.

Licha ya wizara ya fedha kutoa kima cha shilingi milioni sita, kwa ununuzi wa kipande cha ardhi, kiongozi wa mashtaka alisema kuwa hakuna kipande chochote chaa ardhi kilichonunuliwa.

Aidha maafisa hao wakuu katika wizara ya fedha walishtakiwa kwa makosa ya ufisadi, matumizi mabaya ya afisi, matumizi mabaya ya fedha na pia njama za kuiba shilingi bilioni 17. Kwa sasa wizara ya fedha haina uongozi kwani waziri na katibu wake wanakabiliwa na makosa ya kiuchumi.

Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri

Wakati huo huo, mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri yanatarajiwa kufanywa na rais Kenyatta baada ya Rotich kushtakiwa. Rais Kenyatta anatarajiwa kumchagua waziri mmoja ambaye ana imani naye kuwa kaimu katika wizara hiyo ya fedha. Bunge lazima liidhinishe uteuzi huo. Katika hotuba kwa taifa, mwezi wa Aprili  mwaka huu, rais aliwaonya mafisadi

Wakenya wanasubiri kuona iwapo, matamshi ya rais yatakuwa na mashiko, kwani katika siku za nyuma, ameonekana kuwakemea mafisadi bila ya kuchukua hatua mwafaka.

Rais anatarajiwa pia kuteua kaimu katibu mwingine katika wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Susan Jemtai Koech kutiwa mbaroni. Wizara ya fedha ni muhimu katika masuala ya kuendesha serikali na haiwezi kukaa bila uongozi.

Wakati sakata hiyo ilipofichuliwa naibu rais William Ruto, alimtetea Rotich ambaye anatokea eneo lake la Bonde la Ufa. Kukamatwa kwa maafisa hao ambao wengi wanatokea ngome ya siasa ya Ruto kumetikisa chama cha Jubilee ambacho kinazidi kuyumba.

Mabadiliko mengine ambayo yanatarajiwa kufanywa ni pamoja na ya afisa mkuu mtendaji wa Mamlaka ya Mazingira Geofrey Wahungu kukamatwa na kushtakiwa.